Wazungu Wamfuata Chama Simba

Wazungu Wamfuata Chama Simba
SIKU za kiungo mchezeshaji fundi wa Simba, Mzambia, Claytous Chama za kubaki kuendelea kuichezea timu hiyo zinahesabika baada ya kupata ofa katika nchi mbili za Ulaya. Kiungo huyo mwenye uwezo mkubwa wa kupiga pasi zilizonyooka na chenga za maudhi, alitua kuichezea timu hiyo kwenye msimu huu wa Ligi Kuu Bara akitokea Power Dynamos ya nyumbani kwao.



Mzambia huyo, tangu ametua kujiunga na Simba, amempa wakati mgumu kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima ambaye hana nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Mbelgiji, Patrick Aussems. Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, Simba imepokea ofa hizo mbili kutoka Uturuki na Ubelgiji, zote zikimtaka na timu hiyo kuonyesha nia ya kumuachia kwenda kucheza soka huko lakini kwa dau la kufuru.



Mtoa taarifa huyo alisema, Simba baada ya kupokea ofa ya kiungo huyo walimtaarifu meneja wake kutoka nchini Canada, Faustino Mkandila ambaye yeye alitoa masharti ya kumuuza mchezaji huyo akiwa kwenye mkataba. Aliongeza kuwa, sharti alilolitoa kwa Simba kama wanataka kumuuza dau lake ni dola milioni 2 (zaidi ya shilingi bilioni 4.5), hivyo mabosi wa timu hiyo wapo kwenye mazungumzo na meneja huyo.

“Uwezekano wa Chama kuendelea kudumu kuichezea Simba ni mdogo katika msimu huu kutokana na ofa nyingi anazoendelea kuzipata kutoka nje ya nchi. “Zipo nchi mbili kutoka kwa Wazungu ambazo klabu zao ni siri, ni kutoka Uturuki na Ubelgiji tayari zimeleta ofa zao kwa ajili ya kumsajili, hivyo kama mazungumzo yakienda vizuri kati yetu na meneja wa Chama, basi tutamuachia kwenda huko.



“Meneja wake ameleta ugumu katika kumuachia kutokana na dau kubwa analotaka tumuuze ambalo ni dola milioni 2, ambazo ni nyingi lakini mazungumzo yanaendelea,”alisema mtoa taarifa huyo.



Walipotafutwa viongozi wa Simba kuzungumzia hilo akiwemo mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi na Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Crescentius Magori kwa njia ya simu zao za mkononi, ziliita bila kupokelewa.



Vigogo hao wapo Eswatini kwa ajili ya mchezo wa marudiano na Mbabane Swallos wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao ulichezwa jana Jumanne.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad