Wabunge wawili wanaotokea Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, kupitia jimbo la Arusha Mjini Godbless Lema, na Arumeru Mashariki Joshua Nassari wamejikuta kwenye kashfa ya kutoonekana kwenye maeneo yao ya kazi baada ya kulalamikiwa kwa nyakati tofauti.
Godbless Lema ndiye aliyekuwa Mbunge wa kwanza kulalamikiwa kupitia ofisi ya Spika, wakati mkutano wa 13 wa vikao vya Bunge la Tanzania ambapo Spika wa Bunge, Job Ndugai alimtaja Mbunge huyo kwenye orodha ya wabunge wenye mahudhurio hafifu ndani ya bunge pamoja na kamati anazoshiriki.
Kwenye kikao hicho kilichofanyika mwezi Novemba 2018, Spika Job Ndugai alisema Mbunge Lema ana mahudhurio yasiyoridhisha, kuliko wabunge wengine na akifika bungeni mbunge huyo amekuwa hamalizi vikao vyote vya siku.
Kupitia www.eatv.tv, Lema alijibu madai hayo kwa kusema "kwangu mimi bunge limepoteza hadhi sio maamuzi ya wabunge yanayoweza kusababisha mabadiliko ya taifa hili, kwa maana hiyo morali ya kufanya kazi ya kibunge ndani ya bunge inapungua na badala yake inatulazimu kujenga wigo mpana nje ya bunge, ili inapokuja uchaguzi wa 2020 tuwaondoe wabunge wa CCM."
Sakata la utoro halikuishia kwa Mbunge huyo wa Arusha Mjini, pia jana lilimkumba Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari baada ya kutajwa na Mbunge wa viti maalum wa CCM, Amina Mollel kuwa mbunge huyo haonekanai Bungeni.
"Naamini walifanya makosa na hawatarudia tena 2020 na mimi niko hapa kwa ajili ya kuwasemea ili kuhakikisha shida zao zinatatuliwa," Alisema Amina Mollel
Hata hivyo kufuatia madai hayo mara kwa mara uongozi wa CHADEMA umekuwa ukijibu masuala hayo kwa kusema wabunge wake wamekuwa hawapewi mialiko rasmi na viongozi wa serikali, huku wengine wakikabiliwa na kesi mahakamani.