Shirikisho la soka nchini (TFF) kupitia kwa Bodi ya Ligi (TPLB) na kamati ya saa 72, imevitaka vilabu kutojihusisha na vitendo vya kishirikina kama ambavyo vimejitokeza hivi karibuni kwenye mechi mbalimbali zikiwemo zilizohusisha Simba na Yanga.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya ligi (TPLB), Ibrahim Mwayela amesema bodi kupitia kamati yake ya saa 72 inakemea vitendo visivyo vya kiungwana michezoni ikiwemo vinavyoashiria ushirikina ambavyo vimekuwa vikitokea.
Aidha Mwayela amesema kamati imepitia ripoti ya mechi mbalimbali na kubaini kuna matukio yasiyo ya kiungwana kwa mujibu wa kanuni namba 43 ya uendeshaji wa ligi inayoeleza kuhusu udhibiti wa klabu hivyo hata kama vitendo vitafanywa na mashabiki bado klabu itaadhibiwa.
Aidha amesema katika matukio yaliyotokea kwenye mchezo wa Yanga dhidi ya Tanzania Prison klabu hizo zote mbili zimeadhibiwa kwa mujibu wa kanuni huku mchezaji Andrew Vicent wa Yanga akifikishwa katika kamati ya nidhamu ya TFF kwaajili ya kujadiliwa kitendo chake cha kumpiga mwamuzi.
Kwa upande mwingine wachezaji Hassan Dilunga wa Simba na Ibrahim Job wa Lipuli FC wamefungiwa mechi 3 pamoja na faini ya shilingi laki tano (500,000) kwa kila mmoja kutokana na kitendo cha kugoma kuingia vyumba vya kubadilishia nguo wakati wa mapumziko huku wakibaki uwanjani.