Yanga yafanya balaa Mbeya, yavuka mwiba wa kwanza
0
December 04, 2018
Klabu ya soka ya Yanga imeendeleza ubabe wake katika ligi kuu Tanzania bara msimu huu baada ya kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Tanzania Prisons katika uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
Mchezo huo uliotawaliwa na vurugu kadhaa hasa kipindi cha kwanza, ulimalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi huo ikitokea nyuma kufungwa bao moja kwa takribani dakika 75.
Mabao ya Yanga yamefungwa na Ibrahim Ajib katika dakika ya 76, Amis Tambwe katika dakika ya 85 na 90+2 huku bao pekee la Tanzania Prisons likifungwa katika dakika ya 45+2.
Vurugu hizo zilizotokea kipindi cha kwanza, zilizaa kadi nyekundu kwa wachezaji wawili, Mrisho Ngassa wa Yanga na Laurien Mpalile wa Tanzania Prisons baada ya kuhusika na vitendo vya utovu wa nidhamu mara tuu baada ya Tanzania Prisons kupata mkwaju wa penalti. Kadi hizo zilisababisha timu zote mbili kucheza zikiwa pungufu kwa dakika zote za 45 za kipindi cha pili.
Yanga imeendeleza rekodi yake nzuri msimu huu, ambapo mpaka sasa imeshinda michezo 12 kati ya 14 iliyocheza, ikipata sare michezo miwili na kufikisha jumla ya alama 38 kileleni mwa msimamo wa TPL. Yanga inatarajia kucheza na Mbeya City mchezo unaofuata wa ligi kuu Tanzania bara katika harakati za kuzisaka pointi sita mkoani Mbeya.
Tags