BEKI mkongwe na nahodha wa Yanga, Kelvin Yondani amekubali yaishe na kukubali kujiunga haraka na timu hiyo mara baada ya kurejea jijini Dar es Salaam ikitokea Mbeya.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku chache tangu ziwepo taarifa za beki huyo kuweka mgomo akidai amaliziwe fedha zake za usajili na mishahara ya miezi minne.
Beki huyo hakuwepo kwenye michezo mitatu ya Ligi Kuu Bara waliyocheza na Mwadui FC kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Kagera Sugar (Kaitaba), Kagera na Tanzania Prisons (Sokoine), Mbeya.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Yondani alisema kuwa ataanza kufanya mazoezi na timu hiyo iliyotarajiwa kurejea Dar, jana kwa ajili ya mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Biashara United utakaopigwa keshokutwa Jumapili.
Yondani alisema atajiunga na Yanga baada ya kupona majeraha ya enka aliyoyapata akiwa kwenye kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars ilipocheza na Lesotho katika mchezo wa kuwania kufuzu Afcon.
“Tayari nimewasiliana na viongozi wa Yanga akiwemo kocha (Zahera) kumtaarifu kuwa nipo fiti hivi sasa baada ya kupona enka, hivyo timu itakaporejea Dar ikitokea Mbeya nitajiunga nayo kuanza mazoezi kwa ajili ya mchezo ujao wa ligi tutakaocheza na Biashara.
“Mengi yalizungumzwa juu yangu kuwa nimegoma, niwaambie Wanayanga sijaigomea timu, kikubwa kilichonisababishia nishindwe kusafiri na timu ni majeraha yangu ya enka niliyopata nikiwa na Stars,” alisema Yondani.