Katibu wa Itikadi na Uenezi Chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu amesema kwamba muswada wa sheria wa Vyama vya Siasa vipo vifungu vimetengenezwa maalumu kwa viongozi kama kina Nape Nnauye na Hussein Bashe ili kuwawekea mazingira magumu kutokana na yanayoendelea ndani ya chama chao.
Katibu wa Itikadi na Uenezi kushoto, Ado Shaibu Mbunge Nzega Mjini ,Hussein Bashe Katikati na Mbunge wa Mtama Nape Nnauye.
Leo Januari 10 katika kipindi cha East Africa Breakfast ya East Africa Radio, Ado amesema kwamba katika muswada huo kipo kifungu ambacho kinamzuia mtu anayefukuzwa chama chake kuhamia chama kingine na kupewa nafasi ya kugombea.
Aidha amesema kwamba kwa fukuto linaloendelea katika Chama Cha Mapinduzi wao kama upinzani wanahitaji kutumia udhaifu na migongano iliyopo ndani ya chama hicho kama fursa ya kujinufaisha nayo ndiyo maana wanaunga pia kupinga muswada huo wa sheria ya vyama vya siasa.
"Niweke wazi kwamba watu kama kina Nape, Bashe ndiyo wanaowekewa vifungo vya namna hii. Sisi wapinzani tunachukua fursa wao wanavuruga basi na sisi lazima tuwavuruge. CCM kwa kuwa wanajua wanalo fukuto wanatengeneza mazingira ya kuwanyima nafasi za kugombea 2020 endapo watashugulikiwa", amesema kiongozi huyo.