Washtakiwa hao walifutiwa kesi hiyo baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuomba kuondoa shtaka hilo mahakamani hapo na hawana nia ya kuendelea nalo.
Maombi hayo yaliwasilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Hashimu Ngole, kisha mahakama hiyo ikayakubali na washtakiwa wakafutiwa mashtaka yao yaliyowakabili.
Washtakiwa hao walifutiwa kesi hiyo chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.
Ngole alidai mahakamani hapo kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa lakini DPP hana nia ya kuendelea nalo dhidi ya washtakiwa hao.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Augustina Mmbando, alisema shauri hilo lilikuja chini ya kifungu namba 91(1) cha CPA, sura ya 20, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 ila kutokana na maombi hayo, mahakama hiyo imeifuta kesi hiyo.
Hata hivyo, baada ya Hakimu Mmbando kufuta kesi hiyo, washtakiwa hao walikamatwa tena na kuwekwa mahabusu na kisha baadaye kupandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka 39.
Mbali na Yusufali, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Alloyscious Mandago, Isaack Kasanga, Taherali Sujjauddin Taherali na Mohamed Seif.
Wakili Ngole akisoma hati ya mashtaka hayo mapya mbele ya Hakimu Mmbando, alidai kuwa kati ya Machi 2, 2010 na Aprili 26, 2016 katika maeneo tofauti ndani ya Dar es Salaam, washtakiwa hao walikula njama kwa kughushi, kukwepa kulipa kodi na kutakatisha fedha.
Katika shtaka la pili linalomkabili mshtakiwa wa tatu Kasaga, Wakili Ngole alidai kuwa kati ya Mei 9, katika ofisi za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) zilizoko Manispaa ya Ilala, aliwasilisha nyaraka za uongo yenye fomu namba 128 ya Mei 2, 2016 akionyesha kuwa Machi 4, 2012 wakurugenzi wa Kampuni ya Superior Financing Solution Limited ni Yusufali, Kassanga na Maria.
Katika shtaka jingine la utakatishaji fedha kinyume na sheria linalowakabili washtakiwa wote, inadaiwa kati ya Machi 4, 2011 na Aprili 13, 2016 katika maeneo tofauti ndani ya Dar es Salaam akiwa mmiliki na mkurugenzi wa kampuni hiyo walijihusisha na muamala wa kiasi cha Sh 2,967,959,554 wakijua fedha hizo zinatokana na zao la fedha haramu.
Baada yakusomewa mashtaka hayo, Ngole, alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika na wanaandaa maelezo ya mashahidi kwa ajili ya kupelekwa Mahakama Kuu.
Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote, Hakimu Mmbando, aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 24, mwaka huu.