Aliyekuwa Ofisa Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Godfrey Mapuga amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu tuhuma za kumiliki mali ya zaidi ya Sh.milioni 720 ambayo hailingani na kipato chake cha sasa wala cha zamani.
Akisoma hati ya mashtaka jana Januari 19, 2019 ,Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Vitalis Peter akisaidiana na Lilian William amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Salim Ally kuwa, mshtakiwa ametenda kosa hilo kati ya Aprili Mosi mwaka 2011 na Julia 19,2016 huko wilyani Ubungo mkoani Dar es Salaam.
Imedaiwa mshtakiwa akiwa ameajiriwa kwa nafasi ya Ofisa Msaidizi wa forodha wa TRA alikutwa akimiliki mali isiyolingana na kipato chake ambapo, alikutwa anamiliki nyumba ya gorofa moja yenye thamani ya Sh. 698,921,217, kiwanja ambacho hakijasaliwa kilichopo eneo Mbezi Juu,
Ubungo chenye thamani ya Sh. Milioni 7, Kiwanja kingine ambacho hakijasajiliwa chenye thamani ya Sh. 9,500, 000 kilichopo eneo La Goba.Mali nyingine ni kiwanja ambacho hakijasajiliwa chenye katika eneo la Kigamboni Wilayani Temeke chenye thamani ya Sh.milioni sita.
Imedaiwa kuwa mali yote hiyo ina thamani ya Sh. 721,421,217 mali ambayo hailingani na kipato chake cha sasa wala cha zamani. Hata hivyo mshtakiwa amekana kutenda kosa hilo na amerudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Hata hivyo Mahakama imemtaka mshtakiwa kuweka fedha taslimu Sh. 360,710,608 au kuweka mali isiyohamishika yenye thamani ya kiwango hicho cha fedha, pia mshtakiwa ametakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja anatakiwa kusaini bondi ya milioni 360.
Aidha mshtakiwa ametakiwa kuwasilisha hati zake za kusafiri mahakamani hapo na Pia haruhusiwi kusafiri nje ya mkoa wa Dar es Salama bila ya kuwa na kibali.Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo umeishakamilika na imeahirishwa hadi Januari 29,2018 kwa ajili ya mshtakiwa kuja kusomewa maelezo ya awali (PH).