Askofu Kakobe Akana Kumiliki Kadi ya CHADEMA....Awataka Wanaotukana Viongozi wa Dini Wakatubu
0
January 27, 2019
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe amesema yeye na kanisa hilo si wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Pia, amewataka viongozi wa Chadema waliotukana viongozi wa dini watubu hadharani, wasipofanya hivyo, chama chao kitatumbukia kwenye shimo refu zaidi, hawataweza kuinuka tena.
"Baada ya kumalizika kwa mkutano kati ya Rais Magufuli na viongozi wa dini, kuna baadhi ya viongozi wa siasa wa CHADEMA tena walioko katika baraza kuu waliwatukana viongozi wa dini kupitia mitandao ya kijamii, wajue viongozi wa dini wana nguvu katika nchi hii kuliko wao wanavyodhani.
" Viongozi ambao wamewatukana viongozi wa dini kwenye mitandao ya kijamii wanapaswa kutubu haraka sana, wakikaidi agizo hilo chama chao kitatumbukia kwenye shimo refu ambalo hakitainuka tena, kuwatukana viongozi wa dini kwa sababu hawakuzungumza yale mliyotaka kuyasikia ni utovu wa nidhamu ni kiburi", amesema Askofu Kakobe.
Kiongozi huyo wa FGBF ametoa kauli hiyo leo Jumapili Januari 27, 2019 jijini Dar es Salaam wakati wa ibada kufuatia siku za hivi karibuni kuonekana mara kadhaa kwenye hafla za Rais John Magufuli na kupewa nafasi ya kuomba.
Hata hivyo, amesema aliwahi kuhudhuria mkutano mmoja tu wa Chadema uliofanyika Mlimani City na kwamba katika mkutano huo alihudhuria si kama mwanachama bali kama baba ambaye anaweza kualikwa na watoto wengi.
"Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, sijawahi kuwa na mazungumzo naye; iwe kanisani au nyumbani au mahali popote. Hata katika mkutano ule nilipokelewa na viongozi wengine kabisa," amesema Askofu Kakobe.
Amesema hajawahi kuonana wala kuzungumza kwa simu na mbunge wa jimbo la Ubungo (Chadema), Saed Kubenea ambaye anaongoza eneo ambalo kanisa lake lipo.
"Kama hamjui, nimehudhuria mikutano mingi zaidi ya CCM kuliko Chadema. Nakumbuka wakati mmoja niliwahi kuhudhuria mkutano wa wazee kumuaga Rais Benjamin Mkapa, nilialikwa na Yusuph Makamba. Wakati ule nilihudhuria mikutano mingi kwa sababu Makamba ni rafiki yangu sana," amesema.
Askofu Kakobe amesema kuhudhuria kwake mikutano ya Rais Magufuli kumeibua mitazamo tofauti, wengine wakisema ameahidiwa ubunge na wengine wakisema amenunuliwa. Hata hivyo, amekanusha madai hayo.