Klabu ya Azam FC imefanikiwa kutwaa Kombe la Mapinduzi baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba SC, zote za Dar es Salaam katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Gombani, kisiwani Pemba jioni ya leo.
Pamoja na Kombe, Azam FC, timu inayomilikiwa na bilionea Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa imezawadiwa fedha taslimu Sh. Milioni 15, wakati Simba SC wamepata Sh. Milioni 10,000.
Shujaa wa Azam FC leo ni mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa aliyeifungia timu hiyo bao la ushindi dakika ya 82 kwa kichwa akimalizia krosi ya winga Mghana, Enock Atta-Agyei.
kiungo Mudathir Yahya Abbas alianza kuifungia Azam FC dakika ya 44 akimalizia pasi ya winga Mghana, Enock Atta-Agyei.
Beki wa kati, Yussuf Mlipili akaisawazishia Simba SC dakika ya 61 akimalizia vizuri kona iliyochongwa na kiungo Shiza Ramadhani Kichuya.
Hiyo inakuwa mara ya tano na mara ya tatu mfululizo kwa Azam FC kutwaa taji hilo tangu michuano hiyo ianzishwe mwaka 2007, baada ya awali kulibeba katika miaka ya 2012, 2013, 2017 na 2018.
Na hii ni mara ya tatu wanaifunga Simba SC kwenye fainali ya michuano hiyo baada ya 2012 na 2017.