Benki kuu ya Tanzania (BOT) imehamisha madeni na mali zote za Bank M kwenda Azania Bank kutokana na Benki hiyo kushindwa kujiendesha.
Uamuzi wa kuunganishwa kwa benki hizo ulifikiwa Januari 2, 2019 hii ikiwa ni baada ya kuiweka Benki M chini ya uangalizi tangu Agosti 2,2018.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Januari 15, 2019 Naibu Gavana wa BoT, Dk Benard Kibese amesema licha ya kufanyika kwa mikutano mingi kati ya wamiliki, bodi na uongozi ndani ya siku 90 zilizotolewa awali lakini hazikuzaa matunda.
"Tuliwapa muda wa kutosha kujitathmini namna ya kuinusuru benki hii kwa kupata ukwasi wa kutosha lakini ikashindika na ilipofika Novemba 2, 2018 tuliwaongezea siku 60 lakini bado hakukuwa na tumaini," amesema Dk Kibese.
"Kinachofanyika sasa ni mkurugenzi wa Benki ya Azania kuunganisha mifumo na kufungua milango kwa waliokuwa wateja wa Benki M kuanza kupata huduma licha ya kuwa kuanzia leo wale wote wenye madeni watakuwa wanalipia Benki ya Azania,’’ amesema.
Mpaka Benki M inaunganishwa na Benki ya Azania ilikiwa na madeni ya Sh618 bilioni.