Bunge Lasitisha Kufanya Kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)

Bunge Lasitisha Kufanya Kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
Spika wa Bunge Job Ndugai, amesema kwa sasa Bunge limesitisha kufanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.

Kutokana na hali hiyo, amewatawanya wajumbe wa Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Tawala za Mikoa na Mitaa (LAAC) kufanya kazi katika kamati nyingine.

Hatua ya usitishaji huo inatokana na kauli ya Profesa Assad aliyoitoa Desemba mwaka jana katika mahojiano na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Arnold Kayanda.

Mtangazaji huyo alimuuliza CAG kuwa ni vipi ofisi yake imekuwa ikijitahidi kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa ripoti zenye kuonesha kuna ubadhirifu, lakini baada ya hapo wananchi hawaoni kinachoendelea.

Katika majibu yake CAG alisema; “Hilo ni jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge. Kama tunatoa ripoti zinazoonyesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge.

“Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa.

 “Sisi kazi yetu ni kutoa ripoti. Na huu udhaifu nafikiri ni jambo lenye kusikitisha. Lakini ni jambo ambalo muda si mrefu huenda litarekebishika, ni tatizo kubwa ambalo tunahisi Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa.”

Spika Ndugai jana alisema suala hilo si la utani kama baadhi ya wanasiasa wanavyolichukulia.

“Hili jambo sio la utani utani kama hao kina Zitto (Mbunge wa Kigoma Mjini) wanacheza huko Dar es Salaam, sisi hili jambo lililotokea limetusikitisha sana kiukweli.

“Huwezi kutuita sisi dhaifu halafu wewe ni mtu unatakiwa kufanya kazi na sisi.

“Sisi hatutegemei utuite dhaifu yaani kama mazezeta, hiyo ni kuonyesha kwamba si kwamba tumevunja hizo kamati. Ila kwa sasa tumesitisha kazi ya hizo kamati kwa muda. Kwa hiyo wabunge kama wabunge watafanya kazi kupitia kamati nyingine.

“Tumesitisha kwa muda ili hili jambo la huyu ambaye ni mshirika wetu (CAG Profesa Assad) katika kufanya kazi, kwanza afike mbele ya Kamati ya Bunge aeleze kama sisi ni wadhaifu ama laa. Vinginevyo hatuna haja ya kufanya naye kazi ili atafute hao ambao ni ‘strong’ (wenye nguvu) afanye nao kazi.

“Yaani hili si suala la magazeti kama mnavyoandika ushabiki, hatuwezi kujenga nchi ya watu wa kudharaulianauliana, ‘no’ (hapana), haiwezekani.

“Haiwezekani watu mnafanya kazi zenu, watu na heshima zenu mnajitahidi kufanya mnavyoweza, lakini kwa hili acha aje kwanza tumsikilize nini atajibu kwenye kamati, na majibu yake ndani ya kamati mapendekezo yao tutayatoa kwa umma.

“Na kuhusu kamati, ningependa kwanza tubakie huko   maana hili sasa tayari lipo kwenye Kamati ya Maadili, sipendi sana kulirudiarudia, tunataka afike tarehe 21 (Januari) na baada ya hapo mapendekezo yao tutayatoa ‘public’ (kwa umma).

“Kiuweli kuhusu hili la kamati za Bunge tumesitisha kwa sasa shughuli za kamati hizo mbili (PAC na LAAC) mpaka jambo hili litakapokaa vizuri,” alisema Spika Ndugai.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad