Bunge latikiswa na Mauaji


Waziri wa mambo ya ndani Mh. Kangi Lugola, ametoa maelezo juu ya mauaji ya watoto yaliyotokea mkoani Njombe, na kuleta hali ya sintofahamu na hofu kwa wakazi wa mkoa huo


Akizungumza wakati akijibu swali Bungeni, Waziri Kangi Lugola amesema kwamba tukio hilo kweli limeleta taharuki kwa wakazi wa Njombe, lakini jeshi la polisi limeshachukua hatua kuweza kulikabili.

Akiendelea kufafanua zaidi Waziri Lugola amesema kwamba hivi sasa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Hamadi Masauni yuko mkoani Njombe kufanya vikao na kamati za ulinzi na usalama,  kutafuta na kuwachukulia hatua wale waliohusika kufanya matukio hayo ya mauaji kwa watoto wasio na hatia.

“Ni kweli kumekuwa na sintofahamu na taharuki katika mkoa wa Njombe kutokana na vitendo vya baadhi ya watanzania wenzetu, wamekuwa wakichukua watoto wadogo na kuwaua, kuanzia juzi Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamadi Masauni yuko Njombe, anafanya vikao na kamati za usalama za Wilaya na Mkoa kuhakikisha kwamba vitendo hivi vinakomeshwa, lakini taarifa za awali zinaonesha ni imani za kishirikina”, amesema Waziri Lugola.

Waziri Lugola ameendelea kwa kuwataka wabunge kutoa ushirikiano juu ya suala hilo, na kuwapa onyo Watanzania wote kuacha vitendo hivyo vya kikatili.

“Wabunge watupe ushirikiano kwa sababu maeneo yale wanayafahamu vizuri, nitoe onyo kwa Watanzania wote, wasitingishe kiberiti cha serikali ya Rais Magufuli, wasipoacha vitendo hivyo watakipata cha mtemakuni, na tumeshaanza na kule Njombe”, ameongeza Waziri Lugola.

Hivi karibuni kumetokea mauji ya kutisha mkoani Njombe, ambapo watoto wamekuwa wakiuawa kikatili na baadhi kunyofolewa sehemu za siri.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad