China imesema chombo chake kimefanikiwa kutua katika sehemu ya Mwezi ambayo huwa mbali zaidi na Dunia, mara ya kwanza kwa jambo hilo kujaribiwa.
Vyombo vya habari vya serikali ya China vimesema chombo hicho kilichopewa jina Chang'e-4 kilitua mwendo wa saa nne na dakika 26 saa za Beijing katika eneo la Bonde la Aitken upande wa kusini wa Mwezi.
Chombo hicho kimebebea mitambo na vifaa vya kupeleleza eneo hilo, pamoja na kufanya majaribio kadha ya kibiolojia.
Kutua kwa combo hicho kumetazamwa kama hatua kuu katika upelelezi wa anga za juu.
Kumekuwa na safari nyingi sana za vyombo kwenda kwenye Mwezi lakini nyingi ya safari hizo huwa za kwenda kuuzunguka, kupita karibu nao au kutua pekee.
Mara ya mwisho kwa chombo kutua kikiwa na binadamu ilikuwa Apollo 17 mwaka 1972.
Chombo hicho cha Chang'e-4 tayari kimetua picha zake za kwanza za sehemu hiyo ya mwezi, ambazo zimetolewa na vyombo vya habari vya serikali ya China.
Hakuna mawasiliano ya moja kwa moja, na picha na data zimekuwa zikirushwa kwanza kwa mtambo wa satelaiti kabla ya kupeperushwa hadi Duniani.
Awali, safari za Mwezini zimekuwa zikihusisha vyombo kutua sehemu ya Mwezi inayoielekea Dunia, lakini hii ni mara ya kwanza kwa chombo kutua sehemu hiyo nyingine.
Ye Quanzhi, mtaalamu wa anga za juu Caltech, ameambia BBC kwamba hii ndiyo mara ya kwanza kwa China "kujaribu kitu ambacho hakijajaribiwa awali na mataifa mengine yaliyobobea katika safari za anga za juu".
Chang'e-4 ilirushwa angani kutoka kituo cha kurushia satelaiti cha China cha Xichang mnamo 7 Desemba na ilifika kwenye mzingo wa Mwezi mnamo 12 Desemba.
Sehemu ya mwezi inayoelekea Dunia (kusoto) na sehemu hiyo nyingine (Kulia) huwa na tofauti
Chang'e-4 inapaka kupeleleza shimo kubwa lifahamikalo kama Von Kármán, linalopatikana katika sehemu kubwa ya bonde la South Pole-Aitken (SPA) ambalo linaaminika kutokana na kitu chenye nguvu au kikubwa kuanguka kwenye Mwezi zamani sana.
Ni bonde ambalo kipenyo chake ni 2,500km (maili 1,550) na kina chake ni 13km.
Mtalii wa kwanza kwenda kwenye Mwezi atangazwa
Kitu kilichotengeneza bonde hilo kinaaminika kuwa na nguvu sana kiasi kwamba kilipenya gamba la juu la mwezi hadi sehemu ya ndani ambayo kwa Kiingereza kama 'mantle'.
Wataalamu wataelekeza vifaa vya chombo hicho hadi kwenye mawe yaliyotokana na sehemu hiyo ya ndani iwapo yatatambuliwa.
Lengo la tatu ni kuchunguza mawe yaliyovunjwa vipande vipande ambayo yanapatikana sehemu ya juu ya bonde hilo, kwenye uso wa mwezi, kusaidia kufahamu zaidi kuhusu kuumbwa kwa Mwezi.
Chang'e-4 ina kamera mbili na zaidi itakuwa inafanyia utafiti miali nururishi na mawimbi ya redio. Wanasayansi wanaamini kwamba sehemu hiyo ya Mwezi ndiyo bora zaidi kufanyia utafiti kama huo kwa sababu imekingwa dhidi ya mawimbi ya redio kutoka Duniani.