Familia Yapoteza Watoto Watano kwa Kula Samaki Wenye Sumu


Watoto watano wa familia moja wakazi wa Shehia ya Shanake wilayani Micheweni kisiwani Pemba, wamefariki dunia na wengine wawili akiwemo mtu mzima mmoja wamelazwa katika hospitali ya Micheweni wakiendelea kupata matibabu baada ya kula samaki aina ya kasa kibati wanaosadikiwa kuwa na sumu

Daktari wa hospitali hiyo, Mbwana Shoka amethibitisha kuwapokea watoto hao akieleza kuwa mmoja alifariki akipatiwa matibabu.

Daktari huyo alieleza kuwa uchunguzi wa awali wa kitabibu umeonesha kuwa watoto hao walikuwa chakula chenye sumu.

“Tulijitahidi kujaribu kuokoa maisha ya watoto hao na ya wengine ambao wanaendelea na matibabu hadi sasa hospitalini lakini ilishindikana,” alisema Dkt. Shoka.

Amewataja walionusirika kifo baada ya kula samaki hao pamoja na umri wao kuwa ni Chuku Sadiki Shoka (28) na Asmah Makame Ali (12).

Sadiki ambaye anaendelea kupatiwa matibabu ameeleza kuwa walianza kujisikia vibaya na wengine kutapika baada ya kula samaki.

“Baada ya kula chakula kikiwa na samaki aina ya kasa, nilijisikia vibaya na nikaanza kutapika,” alisema Sadiki.

Baba mzazi wa watoto ambaye hajataka jina lake liandikwe amesema kuwa baada ya kumaliza kula samaki na chakula walichokuwa nacho walianza kuona hali ya watoto inabadilika ndipo wakaamua kuwakimbiza katika kituo cha Afya cha Kiyumbuni kuokoa maisha yao.

Naye Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Hassan Abdallah amewataka wananchi kuwa na subira wakati uchunguzi wa tukio hilo ukiwa unaendelea kufanywa na madaktari.

Watoto waliopoteza maisha ni Hafidh Khatib, Hifidh Khatib, Fatma Khatib Ali, Sabra Said, na Hamida Hamad Rashid.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad