Fanya Haya Kufufua Upya Penzi Lako Mwaka 2019
0
January 05, 2019
HERI ya mwaka mpya! Ni jambo la kumshukuru Mungu kuuana mwaka mpya wa 2019 tukiwa wazima wa afya, wengi walitamani kuuona mwaka huu lakini hawakuweza, wengine wameuona mwaka mpya wakiwa na majanga mbalimbali, yote kwa yote, Mungu ashukuriwe kwa kutuwezesha kuuona mwaka mpya.
Ni kawaida ya watu wengi kuanza kupanga mipango mipya kila mwaka unapopinduka, unapopanga malengo yako, usisahau kufanya tathmini juu ya uhusiano wako wa kimapenzi kuanzia mlipotoka mpaka leo namna ya kuuanza mwaka mpya wa kimapenzi.
Ni ukweli usiopingika kwamba watu wawili mnapoishi pamoja kwa muda mrefu, huwa kuna ile hali ya kuchokana na mwisho mnaanza kuishi kimazoea. Hakuna kitu kibaya kama kuishi kimazoea na mwenza wako, unapaswa kuwa mbunifu, kila mara fikiria mambo mapya yatakayoongeza ladha na kulifanya penzi lenu liwe jipya.
Yafuatayo ni mambo yanayoweza kufufua upya penzi lenu na kumfanya mwenzi wako azidi kukupenda.
ANDAA MTOKO WA KUUKARIBISHA MWAKA MPYA
Bila shaka wapo ambao katika Sikukuu ya Mwaka Mpya walifanya mambo mbalimbali kuusherehekea mwaka mpya. Wapo waliotoka kwenda kwenye maeneo ya ibada, wapo walioenda kwenye maeneo ya starehe na wapo pia ambao waliamua tu kutulia majumbani mwao.
Hayo yote yalikuwa ni katika kuukaribisha mwaka mpya. Achana na yote hayo, tambua kwamba ukiachana na maisha ya kawaida, mwaka mpya wa kimapenzi nao unatakiwa kusherehekewa kwa aina tofauti na siyo lazima uyafanye hayo tarehe moja. Hebu jaribu hii, andaa mtoko maalum wa kuukaribisha mwaka, mkiwa wawili tu.
Kama mna watoto, siku hiyo inabidi wawapishe, tafuta sehemu tofauti ambayo hamjawahi kwenda na mwenzi wako na katika mtoko wenu mnapaswa wawili tu, wewe na umpendaye. Kwenda sehemu ya tofauti ambayo hamjawahi kwenda pamoja, husaidia sana kufufua upya hisia za kimapenzi.
Tenga bajeti kidogo kwa ajili ya chakula cha usiku, vinywaji na viburudisho vingine na kama uwezo unaruhusu, mnaweza kwenda hata kwenye hoteli nzuri mkautumia usiku huo pamoja.
MALIZENI TOFAUTI ZENU ZA MWAKA 2018
Jambo lingine la muhimu, ni kutafuta muafaka wa mambo ambayo yalilitingisha penzi lenu kwa mwaka uliopita. Tafuta muda mzuri wa kuzungumza na mwenzi wako, muombe radhi upya kama kuna mambo ambayo ulimkosea kwa mwaka uliopita. Hata kama tayari ulishamuomba radhi siku za nyuma, rudia tena na muahidi kuwa mtu mpya kwa mwaka 2019 na kutorudia ya nyuma.
Imezoeleka hata kama watu walikuwa na ugomvi, mwaka mpya unapoanza hushikana mikono na kuambiana ‘tusahau ya mwaka jana, tuuanze mwaka upya tukiwa wapya’, unatakiwa pia kuyazungumza hayo kwa yule umpendaye. Maajabu ya mwaka mpya unapoanza, ni kwamba ukimuomba radhi umpendaye, atakusamehe na kukubali kuufunga ukurasa wa zamani nakufungua ukurasa mpya kwa mwaka mpya.
PANGENI MALENGO YA KIMAISHA PAMOJA
Hisia za mapenzi huwa zinanoga sana unapogundua kwamba mwenzi wako hana mpango wa kuachana na wewe. Utajuaje kama malengo yake ni kuishi na wewe milele? Ni pale atakapokuwa anakushirikisha kwenye malengo yake ya muda mrefu. Kama kweli unampenda, tenga muda wa kukaa naye mkiwa wawili na kupanga malengo ya kimaisha ya mambo ambayo mnataka kuyafanya kwa pamoja kwa mwaka mpya.
Msiishie tu kupanga kwa maneno, gawaneni majukumu na kila mmoja aanze kufanya yale anayotakiwa kuyafanya ili kutimiza malengo yenu. Fanyeni kila kitu kwa ushirikiano mkubwa. Ukiyafanya haya, utaona jinsi penzi lenu linavyochipua upya mithili ya bustani ya maua waridi ya kuvutia.
Kwa leo ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.
GPL
Tags