Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amemnyang'anya ofisi ya Ubunge, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe baada ya kueleza hajaitumia tangu mwaka 2010.
Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa Chadema amekuwa mbunge wa Hai kwa awamu ya tatu na ofisi hiyo imekuwa ya mbunge na kuwekewa kibao cha ofisi ya mbunge kwa zaidi ya miaka 20.
Ofisi hiyo ipo katika jengo la mkuu wa wilaya hiyo, ambapo pia zipo ofisi za halmashauri ya wilaya ya Hai na sasa itakuwa inatumiwa na idara ya uhamiaji.
Sabaya amesema lengo la Serikali kutoa ofisi kwa mbunge huyo ilikuwa ni kusaidia wananchi lakini ofisi hiyo imekuwa haifunguliwi.
"Tangu mimi nimeteuliwa kuwa Mkuu wa wilaya hapa mwezi wa nane (mwaka jana) ofisi haijafunguliwa sasa kwa kuwa kuna uhitaji wa ofisi muhimu ya uhamiaji nimeamua kuwapa," amesema.
Amesema amepata taarifa pia tangu Mbowe achaguliwe mwaka 2010 hajawahi kuingia tena katika ofisi hiyo kusikiliza kero za wananchi.
"Sijui yupo wapi ila namsikia huko maeneo mengine akifanya vurugu sasa ofisi hii itatumika kusaidia wananchi," amesema.