Mawasiliano ya intaneti yamefungwa katika miji muhimu ya taifa la DR Congo siku moja baada ya uchaguzi mkuu uliocheleweshwa nchini humo.
Kundi la kampeni la mgombea wa upinzani Martin Fayulu liliishutumu serikali kwa kuamrisha kufungwa kwa mtandao ili kusitisha matangazo ya ushindi mkubwa wa mgombea wake.
Waziri wa mawasiliano nchini humo Emery Okundji alisema kuwa hajui kuhusu hali hiyo. Wachunguzi wamelalamikia visa vya wizi wa kura wakati wa uchaguzi huo.
Shughuli ya kuhesabu kura inaendelea, lakini matokeo hayatarajiwi hadi tarehe 6 mwezi Januari.
Rais wa sasa Joseph Kabila anastaafu baada ya miaka 17 madarakani . ameahidi kuhamisha mamlaka kwa njia inayofaa tangu taifa hili lijipatie uhuru wake kutoka kwa Ubelgiji 1960.
Bwana Kabila anamuunga mkono aliyekuwa waziri wake wa maswala ya ndani Emmanuel Ramazani Shadary, ambaye ndiye mgombea wa chama tawala.
Wagombea wakuu wa upinzani ni Martin Fayulu , ambaye afisa mtendaji wa kampuni ya mafuta na Felix Tshisekedi , mwana wa kiongozi wa upinzani Etienne Tshisekedi.
Je tunajua nini kuhusu kufungwa huko kwa mawasiliano ya Intaneti?
katika mji mkuu wa Kinshasa, mtandao umekuwa haufanyi kazi tangu alfajiri huku ukiwa chini katika miji muhimu ya Goma na Lubumbashi.
Kampuni ya huduma za intaneti duniani ilituma ujumbe kwa wateja wake kwamba serikali imeamuru kufungwa kwa huduma hiyo, ripoti za AFP zimesema.
Haki miliki ya pichaREUTERS
Image caption
Takriban wapiga kura milioni 40 waliruhusiwa kushiriki katika zoezi hilo
AFP imesema kuwa wawakilishi wa Vodacom pia wamesema kuwa serikali iliwaagiza kufunga mawasiliano ya intaneti. lakini waziri wa mawasiliano Emery Okundji aliambia BBC alikuwa hafahamu kuhusu hali hiyo.
Je uchaguzi huo ulifanyika kwa njia gani?
Wachunguzi kutoka kanisa katoliki waliripoti zaidi ya visa 100 vya wachunguzi wa uchaguzi kutoruhusiwa kuingia katika vituo vya upigaji kura.
Liliongezea kuwa takriban asilimia 20 ya vituo vya kupoiga kura vilifunguliwa kuchelewa na kulikuwa na ripoti za vituo vya kupigia kura kubadilishwa katika dakika za mwisho.
Wachunguzi wa shirika la Symocel wanasema kuwa zaidi ya maajenti 20,000 walitishiwa na kulalamika kwamba wengi wa wapiga kura hawakupiga kura ya siri.
Katika mahojiano ya BBC bwana Fayulu alilishutumu jeshi kwa kuwalazimisha wapiga kura katika maeneo mengine kumpigia kura bwana Shadary.
Bwana Tshisekedi alimshutumu bwana Kabila kwa kusababisha vurugu katika siku ya uchaguzi ili kutoa sababu za kisheria zitakazomfanya rais aliyepo kusalia madarakani.
Rais Kabila amesisitiza kwamba uchaguzi huo ulikuwa huru na usiopendelea upande wowote.
Rais Kabila alirithi kutoka kwa babaake Laurent Kabila 2001 aliyeuawa, lakini alizuiliwa kuwania muhula mwengine chini ya katiba mpya.
Alitarajiwa kujiuzulu miaka miwili iliopita , lakini uchaguzi huo ulifutiliwa mbali na tume ya uchaguzi baada ya kusema kuwa ilihitaji muda zaidi kuwasajili wapiga kura..
Uamuzi huo ulisababisha ghasia za kisiasa , huku upinzani ukimshutumu Kabila kwa kujaribu kusalia madarakani.
Siku kadhaa kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo, takriban watu milioni 1.26 walitolewa katika sajili za kupiga kura. Tume ya uchaguzi ilisema kuwa uchaguzi hauwezi kufanyika katika eneo la Beni na Butembo kutokana na ugonjwa wa Ebola .
Upigaji kura pia ulisitishwa katika mji wa magharibi wa Yumbi kutokana na utovu wa usalama.
Huduma ya Intaneti yafungwa baada ya uchaguzi wa urais
0
January 01, 2019
Tags