Jaribio Lingine la Al-Shabaab Lazimwa Kenya, wakimbizwa Kama Mbwa Mwizi
0
January 21, 2019
Watu wenye silaha za moto wanaoaminika kuwa wanamgambo wa Al-Shabaab wamefanya jaribio la kuteka eneo la mradi wa ujenzi wa barabara katika eneo la Shimbirey, pembeni mwa mji wa Garissa nchini Kenya.
Kwa mujibu wa Citizen ya Kenya, watu wanne walijeruhiwa katika harakati za kunusuru maisha yao.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Garissa, Richard Kerina ameeleza kuwa jaribio hilo lilidhibitiwa baada ya polisi kufanyia kazi kwa haraka taarifa walizozipata kutoka kwa wananchi.
Mkaazi mmoja wa eneo hilo alilozungumza na vyombo vya habari kwa masharti ya kutotajwa jina, alieleza kuwa watu hao walikuwa wamejihami na bunduki aina ya AK-47 kila mmoja.
Mwanakijiji huyo alieleza kuwa wavamizi hao walimteka mtu mmoja na kumtaka awapeleke kwenye eneo la mradi huo ambao unatekelezwa na kampuni ya ujenzi ya Kichina.
Imeeleza kuwa wananchi walitoa taarifa polisi; na askari wa jeshi hilo waliwahi katika eneo la mradi na kuwasubiri washambuliaji hao.
“Walipokuwa wanakaribia eneo hilo, walianza kupiga risasi hovyo lakini polisi walijibu haraka,” mwananchi mmoja alisema kwa sharti la kutotajwa jina.
Kwa mujibu wa Kamanda Kerina, askari wake walifanikiwa kuzima jaribio hilo la kigaidi ndani ya dakika 15 na magaidi hao walikimbilia kwenye vichaka.
Jaribio hilo lilizua taharuki katika mji wa Garissa ikiwa ni siku chache tangu magaidi wa Al-Shabaab washambulie jengo lenye hoteli ya Dusit2 jijini Nairobi ambapo takribani watu 21 walipoteza maisha.
Tags