Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ramadhani Ng'anzi amesema jana Ijumaa Januari 18, 2019 kuwa watuhumiwa wanne ambao hakuwataja majina yao kwa sababu za kipelelezi wanajihusisha na utengenezaji wa fedha bandia.
Amesema mtuhumiwa wa kwanza alikutwa na noti bandia za dola za Marekani zenye thamani ya dola 500 (zaidi ya Sh 1.1 milioni).
"Huyu mtuhumiwa wa kwanza aliwapeleka askari wetu nyumbani kwake eneo la Daraja Mbili ambako zilikutwa fedha bandia za mataifa mbalimbali," alisema Ng'anzi
Fedha hizo ni dola za Marekani, fedha za Umoja wa Ulaya (Euro), Kenya, Malawi, Zambia, Rwanda na Sudan.
Alisema watuhumiwa wanashikiliwa kwa ajili ya mahojiano na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani.
Katika tukio jingine, Ng'anzi amesema kuwa watuhumiwa wengine wawili ambao ni Kennedy Mbilinyi na Richard Loishiye wamekamatwa kwa kuiba gari aina Harrier lenye namba za usaili T 241 DKC na kujaribu kulivusha mpaka wa Namanga kuelekea nchi jirani ya Kenya.