Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amewasimamisha kazi vigogo watano wa idara ya wakimbizi kwa madai ya kushindwa kutoa taarifa mapema za uwepo wa marobota 1,947 ya nguo zinazodaiwa kuwa ni za jeshi katika kambi za wakimbizi za Nduta na Mtendeli zilizopo mkoani Kigoma.
Waliosimamishwa ni mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi, Harrison Mseke; mkurugenzi msaidizi wa huduma kwa wakimbizi, Deudsdedit Masusu; mkurugenzi msaidizi huduma kwa wakimbizi usalama na operesheni, Seleman Mziray.
Mkuu wa kambi ya Nduta, Peter Bulugu na John Mwita ambaye ni mkuu wa kambi ya Mtendeli.
Lugola ametangaza uamuzi wake huo jana Jumapili Januari 13, 2019 katika mkutano wake na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam.
Alisema nguo hizo za msaada zilitolewa na shirika la Uniqlo la Japan kwa ajili ya wakimbizi wa kambi hizo lakini viongozi wa idara hiyo hawakutoa taarifa mapema kwa viongozi wa wizara.
“Mizigo yote ya wakimbizi inayotolewa lazima ikaguliwe lakini hawa walikaa kimya. Uwepo wa nguo hizo hauleti picha nzuri hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali ipo katika mchakato wa kuwarudisha wakimbizi Burundi," alisema Lugola.
“Kwa vyovyote nchi ya Burundi itakuwa na mtazamo hasi dhidi ya Tanzania baada ya wananchi wake kupewa nguo za kijeshi. Lazima tuwe makini maana tusipofanya hivi tunaweza tukakuta hadi silaha katika misaada.”
Lugola alisema baada ya kuwasimamisha kazi amemwagiza katibu mkuu wa Wizara hiyo kuunda kamati kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo, kuipa siku 10 za kuchunguza.
Lugola ameagiza mamlaka zinazohusika kumchukulia hatua mratibu wa wakimbizi kanda ya Kigoma, Tony Laizer kuhusiana na mchakato huo.
Kangi Lugola awasimamisha kazi maofisa watano Kisa Sare za Jeshi Za Burundi Zilizoingizwa Nchini
0
January 14, 2019
Tags