Katibu Mkuu Wizara Ya Mifugo Na Uvuvi Awashtukiza Suma Jkt Usiku

Katibu Mkuu Wizara Ya Mifugo Na Uvuvi Awashtukiza Suma Jkt Usiku
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amefanya ziara ya kushtukiza usiku majira ya saa 5:30 13.01.2019, kujionea maendeleo ya ujenzi wa jengo la wizara katika mji wa serikali jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Prof. Gabriel mara baada ya kufika katika eneo hilo alikuta ujenzi wa jengo unaendelea kama ambavyo mkandarasi SUMA JKT alivyokubaliana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kujenga jengo hilo kwa saa 24 na kuridhishwa na ujenzi unavyoendelea na kushukuru ushirikiano unaotolewa na wafanyakazi wa wizara.

“Tunaridhika kwa kweli kama uongozi wa wizara ikiwa ni pamoja na viongozi wetu wa kisiasa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Joelson Mpina amekuwa akitutaka kuwa tusilale tufuatilie kama kazi zinafanyika ndio maana leo hii nimeamua kuja usiku, maana unaweza kuambiwa watu wanafanya kazi usiku na mchana kumbe nikilala na kazi huku zinalala.” Alisema Prof. Gabriel.

Aidha Prof. Gabriel amemtaka mkandarasi SUMA JKT kutobweteka kwa kile alichoelezwa kuwa hadi sasa anafanya kazi nzuri katika ujenzi wa jengo la Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kumkumbusha aendelee kufanya kazi kwa kufuata makubaliano yaliyopo katika mkataba waliosaini kwa kujenga jengo hilo kwa ubora na kulikabidhi kwa wakati.

Katibu mkuu huyo pia amesema hatua ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kufikisha huduma ya umeme katika eneo hilo, imesaidia kufanya kazi ya ujenzi kuwa na kasi zaidi na kupunguza gharama ya mafuta ya dizeli ambayo yalikuwa yakitumika kwenye jenereta hususan nyakati za usiku kwa ajili ya kuwashia taa na kusukumia mitambo ya ujenzi.

Prof. Gabriel ameitaja pia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwa ni moja ya wizara ambayo imechimba kisima chake katika eneo hilo na kutumia maji ya kisima kwa ajili ya ujenzi.

Kwa mujibu wa mkandarasi SUMA JKT jengo la Wizara ya Mifugo na Uvuvi linatarajiwa kukamilika mwezi februari mwaka huu na kuanza kutumiwa na baadhi ya watendaji wa juu wa wizara kabla ya kujengwa jengo lingine kubwa katika eneo hilo, ambalo litatumiwa na wafanyakazi wote wa wizara waliopo mkoani Dodoma katika mwaka ujao wa fedha wa 2019/2020.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad