Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam leo Januari 4, 2019, imeahirisha kesi No. 31 ya mwaka 2018, ambayo imefunguliwa na Kiongozi wa ACT Wazalerndo, Zitto Kabwe na wenzake wawili dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakiitaka mahakama kuzuia kusomwa bungeni mara ya pili kwa muswada wa sheria ya vyama vya siasa.
Katika kesi hiyo ambayo vyama 10 vya upinzani vimeungana kufungua jalada hilo mahakamani hapo huku walalamikaji wakiwa ni Zitto, Joran Lwehabula Bashange na Salim Abdallah Rashid Bimani wote wa Chama cha Wananchi (CUF) imeahirishwa hadi saa 8 mchana leo ambapo Mahakama hiyo itatoa uamuzi.
Akitoa maelezo mahakamani hapo, wakili wa Serikali ameiomba Mahakama kuongezewa muda wa siku 21 ili kuwasilisha utetezi wao lakini mawakili wa upande wa utetezi wameomba wapewe siku chache zaidi sababu muswada utawasilishwa bungeni Januari 15, mwaka huu.
Mawakili hao wamesema ili kuzuia muswada kupelekwa bungeni mahakama itoe muda mchache zaidi, na endapo siku 14 zitatolewa basi mahakama imeombwa kutoa zuio kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupeleka muswada huo bungeni sababu serikali ndiyo inayomiliki muswada. .
Kutokana na hoja hizo na nyingine zilizotolewa mahakamani hapo, Mahakama imepanga kutoa maamuzi saa 8 mchana wa leo.
Katika shauri hilo la kikatiba namba 31 la mwaka 2018, waombaji wanapinga kifungu cha 8 (3) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi, kinachoeleza kuwa muswada wowote hauwezi kupingwa mahakamani.
Pia wanapinga muswada huo pamoja na mambo mengine wakidai unakiuka haki za kisiasa za binadamu, kwa kuwa unaharamisha shughuli za kisiasa na kumpa mamlaka makubwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia mambo ya ndani ya vyama vya siasa, yakiwemo ya uongozi.