Kimenuka Congo...Martin Fayulu Apinga Matokeo ya Urais "Hii ni Kashfa Mbaya Sana"

Martin Fayulu apinga matokeo ya urais DRC

Martin Fayulu, mgombea urais wa upinzani DRC aliyeibuka wa pili, ameyakataa matokeo yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi.

Matokeo ya awali yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) yanaonesha Felix Tshisekedi alipata asilimia 38.57 ya kura zilizopigwa na "anatangazwa mshindi mteule wa urais."

Bw Tshisekedi alipata zaidi ya kura 7 milioni naye Bw Fayulu akapata kura takriban 6.4 milioni, huku mgombea wa serikali Emmanuel Ramazani Shadary akimaliza wa tatu akiwa na takriban kura 4.4 milioni.

Bw Fayulu ameambia Idhaa ya Kifaransa ya BBC kuwa: "Hii ni kashfa mbaya sana. Matokeo haya hayana uhusiano hata kidogo na ukweli halisi. Raia wa Congo hawataukubali utapeli kama huu daima. Felix Tshisekedi hakupata kura 7 milioni, haiwezekani. Alizitoa wapi?"

Ameendelea: "Bw Nangaa (mwenyekiti wa CENI) anafuma kitambaa cheusi kwa uzi wa rangi nyeupe. Natoa wito kwa waangalizi wa uchaguzi kuchapisha matokeo yao.

Bw Nangaa na marafiki zake katika FCC [chama tawala] wamekuwa wakichakachua matokeo kumpa 'kikaragosi' wao ushindi."
Awali, alikuwa ameambia kituo cha redio ya Radio France International (RFI) kwamba matokeo hayo ni "mapinduzi halisi kupitia uchaguzi" na akatoa wito kwa waangalizi wa uchaguzi kuchapisha matokeo waliyo nayo aliyosema ni ya kweli.

Nchini DRC hata hivyo, ni kinyume cha sheria kwa mtu mwingine kando na CENI kutangaza matokeo ya uchaguzi.

Wagombea wa upinzani Martin Fayulu (Kushoto) na Felix Tshisekedi (Kulia) wanashindana na waziri wa zamani wa mambo ya ndani Emmanuel Shadary (Kati)
Mshindi mteule wa uchaguzi huo uliofanyika 30 Desemba mwaka jana, Bw Tshisekedi, kwa upande wake ameyafurahia matokeo hayo na kumsifu pia rais anayeondoka Joseph Kabila.

Amemweleza kama "mshirika muhimu kisiasa."

Akiwahutubia maelfu ya wafuasi wake waliokusanyika mji mkuu Kinshasa, Tshisekedi amesema atakuwa "rais wa raia wote wa Congo".

Kumekuwa na tetesi kwamba kucheleweshwa kwa shughuli ya kutangaza matokeo, ambayo awali yalitarajiwa kutangazwa Jumapili, kulitoa muda kwa Rais Kabila na Bw Tshisekedi kuafikiana.


Kanisa Katoliki limesema matokeo rasmi yaliyotangazwa na tume hiyo yanakinzana na matokeo ambayo yameandaliwa na waangalizi wake.

Wamedokeza kwamba Bw Fayulu alipata kura nyingi, kwa mujibu wa takwimu walizo nazo. Baadhi ya kura za maoni zilikuwa zinamuonesha Bw Fayulu akiwa mbele ya wagombea wengine.

Msemaji wa Bw Tshisekedi Claude Lbalanky ambaye amesema siku ya leo ni "siku njema kwa taifa" ameambia BBC kwamba hakuna makubaliano yoyote kati ya Rais Kabila na Bw Tshisekedi.

"Tuna furaha sana, sana sana. Hii ni siku njema kwa DRC. Mnafahamu kwamba maoni ya wananchi yameheshimiwa. Kwa hivyo, tumefurahia sana."

Kuhusu makubaliano, amesema: "Hilo si kweli hata kidogo. Ukweli ni kwamba hauwezi kuwa na kukabidhiana mamlaka bila vyama kuzungumza. Ilipobainika wazi kwamba tungekuwa washindi, tulikwenda kumuona rais anayeondoka Rais Kabila na kuona jinsi shughuli ya mpito inaweza kufanywa kuwa laini. Sawa.

"Tumeshuhudia jambo kama hilo likitokea Afrika Kusini pale (Nelson) Mandela alipochukua mamlaka kutoka kwa utawala fidhuli wa ubaguzi wa rangi. Ni lazima kuwe na mazungumzo ya aina fulani, kusema 'ehee, nyinyi mmeshinda. Nitakuwa salama?'. Kwa hivyo, bila shaka hakukuwa na zaidi ha hayo. Kwa hivyo, hakukuwa na makubaliano yaliyoathiri matokeo yauchaguzi."

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad