Kisa Lissu, Ndugai 'ashambuliwa'
0
January 31, 2019
Baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kueleza kwamba Bunge limeshamlipa Tundu Lissu Sh250m, kati ya hizo Sh207.8m ni stahiki zake na Sh43m ni mchango wa matibabu ya mbunge huyo, wabunge na viongozi wa CHADEMA wamecharuka na kueleza kwamba pesa hizo ni mishahara yake na siyo hisani.
Mapema leo Ndugai alisema kwamba kuanzia sasa ataanza kumjibu mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kwa kuwa ana amini amepona na kwamba tayari ameshalipwa Sh250milioni kutoka bungeni.
Kauli ambayo ilizua utata ilimfanya Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini kuhoji ni, "mbunge gani ambae hakupewa mshahara na jimbo 'allowance' wakati akitibiwa ajitokeze. Kwanini Lissu asimangwe"?.
Selasini ameongeza kwamba, "msimamo wa Serikali na Bunge ni kutolipa matibabu ya Lissu hoja ikiwa hakupata rufaa ya Muhimbili. Msimamo huo upo kwa barua za bunge kwa familia na chama. Fedha anazosema Spika ni mishahara posho ya jimbo. Wabunge wote hata Spika akiugua mishahara na posho haisitishwi".
Lema ameongeza kwamba "mshahara wa Mbunge sio hisani ya Spika".
Spika Ndugai katika kipindi cha maswali na Majibu alisema kwamba sasa yupo tayari kumjibu Lissu kwa kuwa alikuwa amelala kitandani, na kwamba sasa hivi anaamini kwamba amepona ndiyo maana anafanya ziara.
“Siku za mwanzo sikutaka kujibu maana niliamini kumjibu mtu aliyelala kitandani siyo vizuri kwani kuna vitu huenda vingekuwa vimempita, lakini sasa naamini ni mzima hadi anafanya ziara nje. Nalisema hili akijibu nakuja na mkeka hapa,” amesema Ndugai.
Aidha Ndugai ameeleza kwamba Lissu amekuwa akilalamika kila wakati kuwa Bunge halimjali kitu ambacho hakina ukweli ndani yake na hakuna madai kama hayo.
Tags