Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Antiphas Lissu amemlalamikia Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kwa kushindwa kutimiza ahadi yake ya kwenda kumuona hospitalini kama alivyoahidi kwenye moja ya chombo cha habari nchini.
Lissu ameyasema hayo kupitia Waraka huo wenye kichwa cha habari ‘Mwaka mpya 2019, Mwaka wa kurudisha demokrasia, haki za binadamu na utu wetu Tanzania’ Lissu amelalamika kutotembelewa na Spika wa Bunge, Job Ndugai wala watumishi wa Bunge licha ya kuahidiwa.
“Hadi ninapoandika maneno haya, bado Spika Ndugai hajatimiza ahadi yake hiyo. Hakuna mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge, au Afisa yeyote wa Bunge, aliyefika hospitalini kuniona na kunijulia hali,” amesema.
Aidha kiongozi huyo amelalamika tangu kushambuliwa na watu wasiojulikana kwa risasi Septemba 7, 2017 hakuna mtu yoyote aliyehojiwa na wapelelezi wala Jeshi la Polisi kutofanyia uchunguzi shambulio hilo.
“Katika shambulio hili, hakuna anayeshukiwa na Jeshi letu la Polisi hadi sasa. Hakuna aliyehojiwa na wapelelezi mahiri wa Jeshi letu la Polisi. Hakuna aliyekamatwa na kwa hiyo, hakuna aliyeshtakiwa” alidai Lissu.
Katika waraka wake huo, Lissu amesema anaendelea vizuri na matibabu, kwa sasa ameanza mazoezi ya kutembea bila magongo.
Lissu Amemlalamikia Spika wa Bunge Kushindwa Kutimiza Ahadi Yake
0
January 07, 2019
Tags