Mbunge wa Mtera (CCM), Livingston Lusinde ‘Kibajaji’ amelitaka Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kuacha ubabaishaji kwa wasanii vinginevyo Serikali iwakanye.
Lusinde amesema Basata inawaonea wasanii na kuwafanya waishi maisha ya hofu na ubabaishaji wakati vipaji wanavyo na miiko ya kazi zao wanaijua.
Mbunge huyo amesema hayo kipindi ambacho Basata imewafungia wasanii Naseeb Abdul ‘Diamond’ na Rayvanny kutofanya onyesho lolote ndani na nje ya nchi kwa muda usiojulikana kutokana na kuonyesha dharau na utovu wa nidhamu kwa mamlaka zinazosimamia sanaa nchini.
Mbunge huyo ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM alisema kinachomkera ni Basata kumfungia Diamond kwa ajili ya wimbo wa Mwanza ambao amesema hauna maana mbaya kwani Mwanza kuna kata inaitwa Nyegezi.
Akizungumza na Mwananchi jana, Lusinde aliwataka wasanii na vijana kuungana na kuipinga Basata ambayo amesema si rafiki kwa maendeleo na ubunifu wa wasanii wa Tanzania.
Alisema atapeleka muswada bungeni ili kuangalia utendaji wa chombo hicho na ikibidi kibadilishiwe majukumu ya kutakiwa wao ndiyo wafanye kazi ya kutunga nyimbo na kuwapa wengine waimbe. “Sina amani kwa kuanza mwaka mpya, nakerwa na Basata, hivi vijana wamewakosea nini lakini maana fungiafungia kwao ndiyo mpango, hebu tuwatungie sheria wawe watunga nyimbo wao halafu wasanii waimbe tu, binafsi namkubali sana Diamond,” alisema Lusinde.
Aliitaka Serikali iingilie kati kwa kuwazuia na kuifuta kata ya Nyegezi kwani inapoimbwa inaonekana kuwa matusi. “Waje niwape orodha ya nyimbo za matusi lakini sio wafungiwe kwa wimbo huo, sasa huyu kawafanya nini kama si maonezi tu, waache tabia za maonezi,”alisema.
Lusinde amewataka wasanii kutokatishwa tamaa na baraza hilo badala yake wasonge mbele na ubunifu wao kwani bila kufanya hivyo wataua vipaji vyao na kurudisha nyuma maendeleo yao.
Mwananchi
Kamwe siungi mkono matusi ya aina yoyote yafanywayo na msanii yoyote. Ila sioni km Basata imekaa vema kiutendaji. Nilifikiri Basata ingekuwa ya pili nyuma ya wizara ya utalii katika kuliingizia taifa pato na fedha za kigeni. Tanzania ina tamaduni nyingi mno ambazo zikifanyiwa ubunifu tu ni kivutio tosha kwa watalii. Staili za dansi toka kwa makabila 120 zingeweza kuvuta wasanii wa nataifa mengine kuja na kujifunza kutoka Tanzania. Basata itengeneze index kuzuia mgogoro na wasanii. Pia ifanye kazi zaidi kuliongezea pato taifa, ubunifu zaidi unatakiwa ndani ya Basata.
ReplyDelete