Makala: Inaaminika bundi ‘aliyetua bungeni’ ni tiba kiboko, dawa ya vita, mkosi…


Taharuki, tafakuri, mijadala, utani na sintofahamu ilizuka jana baada ya bundi kuwahi namba ndani ya ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kujitwalia eneo la juu akisoma kila namba ya viti vya waheshimiwa.

Kupitia makala hii fupi, utafahamu mambo mengi ya kustaajabisha kuhusu bundi. Ni ndege ambaye amefanya mengi kwenye hii dunia, ametukuzwa sana hadi picha yake kuwekwa kwenye pesa, ametumika vitani. Amewahi kuaminika kuwa chanzo cha busara na hekima. Pia, amewahi kuwa alama ya bahati na unabii.

Sio hayo tu, amewahi kuaminiwa na ‘wahenga’ kuwa ni chanzo cha tiba kiboko ya ulaibu na ulevi wa kutupwa.

Lakini kwa upande mwingine wa sarafu, ni ndege anayeogopwa sana kuwa chanzo cha mikosi, ishara ya kifo, uchawi/ushirikina, na majanga ya aina mbalimbali.

Kabla sijakueleza hayo, vuta pumzi kidogo nikukumbushe sintofahamu iliyoibuka jana bungeni.

Maafisa wa Bunge waliamua kuhangaika na bundi mapema kabla hajatia doa kibarua chao kwani mgeni huyu hata kitabu cha wageni hajasaini!

Lakini eti naskia… jitihada za kumtimua yule bundi ndani ya Bunge ziligonga mwamba, aliwachezesha michezo ya kuhamahama hadi wakaamua wafanye mambo mengine kwanza. Eti, baadaye akapotea bila kujulikana alitoka vipi mle ndani. Makubwa!

Baada ya Spika Job Ndugai kuingia, aliwatuliza wabunge kuwa ndege huyo hana madhara anapoonekana mchana, kwa Dodoma. Wagogo tupo?!

“Waheshimiwa wabunge, asubuhi tumeanza kumuona bundi ndani ya jengo hili. Lakini kwa Dodoma, Bundi wa mchana hana madhara kwa hiyo ni mambo ya kawaida kabisa,” alisema Spika Ndugai.

Hata hivyo, inasemekana bundi yuleyule, alionekana tena; na wakati huu ulikuwa wa giza kidogo. “Kwani huyu sio yule wa mchana ambaye hana madhara!!?” aliuliza kiutani mtumiaji mmoja wa mtandao wa Twitter.

Je, bundi ana maana gani kwenye historia na imani?

Bundi amekuwa akihusishwa na mambo tofautitofauti. Kuna jamii zinazomkumbatia na kumtukuza ndege huyu; na zipo jamii ambazo zinasali sio tu kwamba zisimuone, bali hata zisisikie sauti yake.

Historia ya imani za aina yake kuhusu bundi ilianza miaka mingi kabla ya kuzaliwa kwa Kristo, ikihamishwa kwa vizazi kwa kutumia masimulizi ya mdomo.

Enzi hizo, huko nchini India na Ugiriki, bundi alikuwa anaheshimiwa.  Alichukuliwa kama chanzo cha amani. Alikuwa ni ishara ya hekima na utabiri wa maisha mema ya usoni, kwa mujibu wa mtandao maalum wa maisha ya bundi wa ‘The Owl pages’.

Katika masimulizi ya kale ya Ugiriki, punde tu baada ya mwaka 499 BC (Kabla ya kuzaliwa Kristo), kiongozi wa Ugiriki aliyefahamika kama muungu wa hekima (Goddess of wisdom), alimuinua bundi na kumpa heshima kubwa. Aliamini bundi ni ishara ya ushindi na mafanikio. Hivyo, alimlinda kwa gharama yoyote na ilikuwa mwiko kwa mtu yeyote kujaribu kumnyima amani ndege huyo.

Bundi alichukuliwa kama mlinzi wa Ugiriki, aliyeongozana na jeshi na kuleta ushindi katika vita.

Ilikuwa hivi, endapo bundi ataruka juu ya jeshi la Ugiriki wakati wa vita, iliaminika kuwa ni ishara kwamba watashinda vita hiyo; na kweli historia inasema walishinda kila ishara hiyo ilipotokea.

Pia, waliamini kuwa bundi anaweza kulinda uchumi wa nchi hiyo. Hivyo, waliweka picha ya ndege huyo katika upande wa pili wa sarafu yao ya fedha.



Lakini mambo yalikuwa tofauti kabisa kwa Dola ya Kirumi. Warumi waliamini bundi alikuwa ishara ya majanga na matatizo makubwa ikiwa ni pamoja na vifo.  Wakati Ugiriki waliamini bundi ni ishara ya ushindi wa vita, Jeshi la Kirumi lenyewe lilionywa kuwa bundi ni ishara ya kushindwa vita.

Inaelezwa kuwa Jeshi la Warumi liliwahi kuonywa kuhusu ishara ya bundi kuruka juu yao kabla ya kuingia vitani; na kwamba walipokea kipigo kikali kutoka kwa maadui baada ya kumuona bundi juu ya anga lao kwenye eneo la Charrhea, katikati ya mito Euprates na Tigris.

Kitabu cha historia iliyomlenga bundi kiitwacho ‘Owls in Lore and Culture’, kilichoandikwa na mtaalam wa historia, Bruce G. Marcot, kinaeleza kuwa Warumi waliamini bundi ni ishara ya kifo.

Inaelezwa kuwa bundi alilia juu ya nyumba ya mwanasiasa na mpiganaji hodari wa jeshi la Kirumi, Julius Caesar na baada ya siku chache aliuawa.  Vivyo hivyo, sauti ya bundi ilisikika karibu na jumba la kifalme la mtawala wa Roma, Commodus na December 31, 192 AD (Baada ya kuzaliwa Kristo) yaani siku chache baadaye aliuawa. Aina hiyo ya utangulizi wa vifo imeripotiwa kwa viongozi wengine waandamizi wa Roma kama Marcus Vipsanius Agrippa na Augustus.

Kwa mujibu wa mtabiri maarufu aliyeishi karne ya pili, Artemidorus, kumuona bundi ndotoni ni ishara kuwa kama una safiri utaporwa au kutekwa nyara. Aliamini kuwa wachawi hujigeuza kuwa bundi hasa nyakati za usiku.

Ingawa Uingereza pia walikuwa na imani yenye mfanano na ile ya Warumi, kulikuwa jambo jema zaidi kuhusu bundi kuwa anaokoa maisha. Kwao bundi alikuwa chanzo cha dawa kiboko ya ulevi pamoja na kifua.

Waingereza wa Karne ya 12, walitumia yai la bundi kumtibu mtu aliyeshindikana kwa ulevi na kumsaidia kuachana na ulaibu huo. Waliamini pia kuwa mtoto anayepewa yai la bundi hatakuwa mlevi ukubwani. Lakini tiba hiyo kwa mtoto chanzo chake kilikuwa kutibu kikohozi sugu.

Mhubiri maarufu aliyewahi kuishi katika karne ya 12 huko Uingereza, Odo wa Cheriton alidai kuwa kumuona bundi ni ishara ya bahati kwani alitengwa na ndege wenzake kwa kosa la kuiba ua waridi alilokuwa anapelekewa mtoto wa kike mrembo wa familia ya kifalme (beautiful princess) na sio vinginevyo. Wahubiri nao huwa wana vistori vitamu kama Wahenga!



Deane Lewis, mfuatiliaji wa masuala ya historia ya wanyama na ndege na mpiga picha maarufu wa wanyama, ameeleza kuwa huko Marekani na India kulikuwa na mchanganyiko wa fikra na imani kuhusu bundi. Wengine wakiamini ukiota bundi ni ishara ya kifo, na wengine wakiamini ni bahati pia.

Haujashangaa bado! Bruce Marcot, alipofanya ziara ya kutafuta historia na imani ya jamii mbalimbali kuhusu bundi, katika kitabu chake cha ‘Owl in Lore and Culture’ anasema mwaka 2007 aliitembelea Hifadhi ya Taifa ya Assam, Kaskazini Mashariki mwa India na aliambiwa kuwa katika jamii yake, wakisikia sauti ya bundi wa aina fulani ya bara Asia akilia, basi wanaamini kuwa kuna msichana mmoja amebalehe au amevunja ungo hivyo inakuwa ni sherehe na vificho kwao.

“Msichana mmoja aliiga sauti ya bundi huyo wa asili ya bara Asia na aliniambia sauti hiyo ni nadra kuisikia, na ikisikika basi huwa ni shangwe na furaha kwani kuna msichana amevunja ungo na atafanikiwa katika maisha,” Marcot alisimulia.

Jamii hii pia hawana shida na bundi, wao wanamuona kama ishara ya baraka na kheri.

Kwa jamii ya Afrika Mashariki, vitabu vya watafiti pamoja na masimulizi ya wahenga wanaamini kuwa bundi sio ishara nzuri sana. Na huko Afrika Kusini, Wazulu wao wanaamini kuwa bundi ni ndege wa waganga wa kienyeji.

Lakini hivi sasa bundi anatunzwa kwenye majumba ya kihistoria huko Afrika Kusini na anakuwa chanzo cha kuingiza fedha kutoka kwa watalii.



Je, wanaomzunguka bundi huyo wao wanahusika vipi na baraka au laana zake? Watalii wao wanalipa ‘mapesa rundo’ wakacheze na bundi wa Afrika Kusini.



Wanasayansi nao wana yao, wao wanaamini bundi ana uwezo mkubwa wa kunusa seli za mwanadamu. Hii naomba niiache kwa leo tubaki kwenye imani zetu kwanza.

Taasisi ya Afrika Kusini inayoshughulikia mazingira na wanyama ya ‘National Zoological Gardens (NZG), imeamua kutenga wiki moja kila mwaka, maalum kwa ajili ya kuelimisha jamii kuhusu faida za bundi kwa mazingira. Lengo ni kuondoa kile wanachoamini kuwa ni imani potofu kuhusu bundi.

Kwa Tanzania, kila mmoja na imani yake, na kabila lake na dini yake wanaamini wanachoamini. Je, wewe unaamini nini kuhusu bundi?

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad