MAKALA: Ni Salamu za Mwaka Mpya Kutoka kwa Hamisa Mobetto Hadi Jokate Mwegelo



Je, Unamkumbuka mrembo Charity Mwangi kutoka nchini Kenya?, ni yule aliyeonekana kwenye video ya kundi la Sauti Sol unayokwenda kwa jina la Shake Yo Bam Bam iliyotoka mwaka 2014. Baada ya hapo mrembo huyo aliweza kushinda taji la Miss World Kenya kwa mwaka 2014.

Vipi kuhusu mrembo wa Kitanzania Carolyne Benard, huyu naye mara baada ya kuonekana kwenye video ya Damian Soul iitwayo Ni Penzi, alienda kushinda taji Miss Universe Tanzania 2014.

Ipo hivi, kuna uhusiano wa karibu sana kati ya warembo wanaonekana kwenye video za muziki (video vixen) na kushinda kwenye mashindano ya ulimbwende. Mwanamitindo Hamisa Mobetto ni mfano mzuri katika hilo ila kwa leo anataka kutuma salamu za mwaka mpya kwa Jokate Mwegelo, kivipi?.

Hamisa na Salamu Zake

Kwa mara ya kwanza Januari mosi mwaka huu ambayo ilikuwa ni sikukuu ya mwaka mpya, Hamisa Mobetto alitumbuiza jukwaani hapa Bongo baada ya mwaka jana kutoa nyimbo mbili ambazo ni Madam Hero na Tunaendana.

Hamisa aliachia nyimbo hizo kwa mashabiki wake na  kwenye vyombo habari lakini hakufanya show yoyote Bongo zaidi ile aliyofanya Marekani akisindikizana muimbaji Christian Bella.
Katika jukwaa alilopanda Hamisa Mobetto kwa mara ya kwanza lilikuwa na waimbaji wakali Bongo kama Lady Jaydee, Ruby, Aslay na Christian Bella, hivyo ni mwanzo mzuri kwake.

Hata hivyo kabla ya Hamisa kuingia kweye muziki alishiriki mashindano kadhaa ya ulimbwende, baaada hapo akaingia kwenye mambo ya Mitindo ambapo alijipatia umaarufu mkubwa na kushinda tuzo na mataji mbalimbali. Haikuishia hapo alionekana kwenye video kadha za Bongo Fleva ikiwa ni pamoja n kucheza filamu.

 Mwaka 2010 Hamisa Mobetto alitwaa taji la Miss XXL, After School Bash, taji ambalo lilikuwa likiandaliwa na kituo cha Radio Clouds FM, na hapo ndipo ukawa mwanzo wa yeye kuamini katika urembo. Mwaka uliofuata (2011) alishiriki mashindano ya Miss Dar Indian Ocean na kushika nafasi ya pili, pia mwaka huo alifanikiwa kuwa Miss Kinondoni namba mbili.

Mwaka 2012 alishhiriki mashindano ya Miss University Afrika na kuingia kwenye orodha ya warembo 10 bora. Huyo ndiye Hamisa linapokuja saula la urembo, ana historia yake kwa kiasi chake, si haba.

Mwaka 2013 alionekana kwenye video ya wimbo wa Quick Rocka uitwao My Baby ambao aliwashirikisha Marehemu Ngwea pamoja na  Shaa, na hapo ndipo ukawa mwanzo wa yeye kuingia masuala hayo (video vixen).

Alikuja kujipatia umaarufu mkubwa mwaka 2016 alipoonekana kwenye video ya Diamond Platnumz inayokwenda kwa jina la Salome akiwa amemshirikisha Rayvanny. Tunaweza kusema haya ndio mafanikio ya juu kabisa kwa upande wa video vixen kwani baaada ya hapo hajaonekana tena kwenye video ya muziki na hana mpango kufanya hivyo.

Hivyo utaona ni kwa kiasi gani urembo, mitindo na muziki vinavyoingilia, ndipo tunarudia awali kabisa nilipowazungumzia kina Charity Mwangi na Carolyne Benard, tuendelee na salamu hizi.

Salamu Zimechelewa

Kama nilivyotangulia kueleza kuwa mwishoni mwaka jana ndio Hamisa aliotoa nyimbo zake mbili na Januari mosi mwaka huu ndipo akapanda jukwaani kwa mara ya kwanza. Mrembo huyo aliwahi kukaririwa akieleza kuwa alipenda sana kufanya muziki tangu utoto kabla ya mengine yote aliyofanya.

Mwaka 2013 alishiriki kwenye wimbo wa Diamond Platnumz uitwao Nikifa Kesho ingawa hakutajwa kama alishiriki kitu kinachopelekea wengi kutofahamu hilo. Hamisa alifanya back vocal kwenye wimbo huo, kwa lugha rahisi ni kwamba sauti mwanamke inayosikika kwa mbali au nyuma ya ile ya Diamond, ni ya Hamisa.

Ukiangalia kutoka mwaka 2013 hadi 2018 ni kipindi kirefu zaidi, pengine alikuwa na nafasi nzuri zaidi ya kufanya muziki kuliko sasa, kwanini?.

Ukiangali kutoka mwaka 2018 hadi 2018 kuna warembo wengi walikuwa wakitokea kwenye video na baadaye kuingia kwenye muziki na sasa wanafanya vizuri na hata kupewa show kubwa na za maana.

Miongoni mwao ni Gigy Money na Amber Lulu, ingawa hawa hawakupita kwenye mashindano ya ulimbwende ila walianzia kwa upande wa video vixen ambapo tunaweza kusema ni hatua mbili nyuma ya Hamisa lakini wamekuja kutoboa ghafla kwenye muziki.

Hata hivyo kwa kipindi hicho (2013-2018) Hamisa hakuwa mtu bure, tunafahamu huyu ni mama wa watoto wawili, hivyo tunaweza kusema malezi pia yalichukua muda wake mwingi, weka hilo kando.
Kwa miaka miwili mfululizo Hamisa Mobetto ameshinda tuzo ya Starqt ambazo hutolewa nchini Afrika Kusini. Starqt Awards ni tuzo zinazohusisha biashara, mitindo, burudani na vitu vingine.

Mwaka 2017 alishinda kupitia kipengele cha People Choice Awards, pia aliwania kwenye kipengele cha Super Mum, hivyo utaona kwa kipindi hicho kuna kazi kubwa aliyoifanya nje ya muziki wake.

Hamisa ana kila sababu ya kutuma salamu za mwaka mpya kwani mwaka uliomalizika (2018) ulikuwa wenye mafanikio makubwa sana kwake kwa upande wa muziki ukiachana na hizo nyimbo mbili alizotoa.

Hivi unafahamu kuwa sauti ya mwanamke inayosikika kwenye wimbo wa Diamond Platnumz akiskirikiana na Mbosso na Lava uitwao Jibebe ni ya Hamisa Mobetto?. Ndiyo, sauti inayosikika ikisema ‘I like’ ni ya mrembo huyo ingawa mwenyewe na wenye wimbo hawapendi sana kuliweka wazi hilo pengine kutokana na makubaliano yao.

Mara kadhaa nimewahi kuona Alicia Keys akitumbuiza kwa kuimba tu chorus ya wimbo wa Jay Z uitwao Empire State of Mind, wimbo huo walifanya pamoja ambapo Alicia Keys ndiye aliyeimba chorus hiyo. Hivyo Hamisa alikuwa ana uwezo wa kuonjesha mashabiki wake kipande hicho tu alichoimba wakati akitumbuiza iwapo hilo lilikuwepo toka awali kwenye makubaliano yao.

Kwanini Jokate 

Mwaka 2006 Wema Sepetu alishinda taji la Miss Tanzania, huku Jokate Mwegelo ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe akishika nafasi ya pili. Baada ya hapo Jokate aliendelea kufanya vizuri kwa upande wa mrembo na mitindo.

Ukija hadi mwaka 2013 Jokate alijinyakuliwa tuzo kutoka Swahili Fashion Week Awards kama Female Stylish Personality, hii ilishirikisha wote wenye umri chini ya miaka 30, pia mwaka 2015 alishinda tuzo hiyo tena kupitia kipengele cha Baileys Female Stylish Personality.

Kabla ya Jokate aliweza kusikia kwenye muziki wa Bongo Fleva kwa kutoa nyimbo zake binafsi na kushirikishwa na wasanii wengine. Miaka mitano iloyopita alitoa wimbo uitwao Kaka Dada akishirikiana na prodyuza wa muziki Bongo, Lucci, pia alitoa wimbo uitwao Leo Leo akimshirikisha Ice Prince kutoka Nigeria.

Pia ameshirikishwa kwenye nyimbo za AY ambazo ni King na Queen iliyotoka miaka nane iliyopita. Wimbo mwingine ni El Chapo ambao kwa bahati mbaya Jokate hakuonekana kwenye video ya wimbo huo.

Hadi kufika hapo utaoka ni kwa kiasi gani Hamisa na Jokate kuna vitu walikuwa wanaenda kuanzia kwenye urembo, mitindo hadi kwenye muziki. Lakini mwaka 2019 unaaza Hamisa akiwa kwenye muziki wake, huku mwenzake akiwa kama Mkuu wa Wilaya na sasa vigumu kurudi nyuma.

Wote hawa ni vijana wa Kitanzania wanaopigania kile wanachokiamini kinawafaa kwenye maisha yao na kila mmoja amefika hapo alipo sasa kutokana na kusimamia kile alichokiamini. Uzuri ni kwamba wote ni marafiki wakubwa kwa sasa, hivyo bila shaka salamu hizo za mwaka mpya zimefika.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad