Mambo 4 yaliyoiangamiza Simba, DR Congo


Unaweza kusema kuwa wengi walitarajia kuwa Simba asingeweza kutoka na matokeo mazuri katika mchezo wake wa jana lakini pia wengi hawakutarajia kuwa angeweza kufungwa mabao 5-0.


Lakini yote mawili yamewezekana na hivyo ndivyo mpira wa miguu ulivyokuwa na utofauti mkubwa na michezo mingine, anayeweza kupanga vizuri mbinu zake ndani ya dakika 90 ndiye anayeshinda.

Haya hapa ni mambo manne ambayo yameigharimu Simba katika mchezo wake wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya  AS Vita Club.

Matumizi ya nguvu

AS Vita walikuwa bora sana katika kutumia nguvu, viungo wa Simba hawakuwa na nguvu ya kupamabana na viungo wa AS Vita na washambuliaji wake. Namna ambavyo Fabrice Luamba, Munganga Omba na Ngonda Muzinga walivyokuwa wakiwasumbua viungo wa Simba, Mzamiru Yassin, James Kotei na Jonas Mkude, ilikuwa ni sababu mojawapo iliyopelekea kupoteza mchezo.

Umakini na mipira ya juu

Hili ni eneo ambalo wachezaji wa Simba hawakuwa bora katika mchezo wa jana. Bao la pili na la nne ambayo yalifungwa kwa kichwa na Bopunga Botuli (19') na Makwekwe Kupa (71') yalionesha udhaifu huo dhahiri, kwani wachezaji hao waliruka na kufunga kirahisi kabisa huku wachezaji wa Simba wakiwa wamesimama.

Umakini wa mabeki

Mabeki wa Simba hawakuwa na umakini wa kutosha katika mchezo wa jana, walizidiwa ujanja na kasi na washambuliaji wa AS Vita, mara nyingi walionekana kuzidiwa kasi na umakini. Hiyo imeonekana katika bao la kwanza na la tatu la penalti.

Kushindwa kubadili mfumo 

Simba walicheza kwa staili ya pasi fupi ambayo haikuonekana kufanya kazi, kwani mara zote pasi hizo zilikuwa zikizuiwa na wachezaji wa AS Vita ambao staili yao ya pasi ndefu iliwasaidia kupata matokeo hasa ukizingatia kuwa mabeki wa Simba hawakuwa bora katika kuwazuia washambuliaji.

Baada ya matokeo hayo, sasa Simba inasalia na alama 3 ikiwa katika nafasi ya tatu huku kundi hilo likiongozwa na Al Ahly yenye alama 4 baada ya kutoka sare na JS Saoura katika mchezo wa pili.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad