Mapunda Asema Muswada vyama vya Siasa Utanyoosha Wahuni


Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda amesema kuwa Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa unaojadiliwa Bungeni umelenga katika kuimarisha demokrasia ya nchi na demokrasia ya vyama; pamoja na kufuta uholela na uhuni.

Akichangia mjadala wa muswada huo leo Bungeni jijini Dodoma, Mapunda amesema kuwa sheria hiyo imeletwa kutokana na uzoefu wa miaka 26 wa uendeshaji holela wa vyama vya siasa nchini pamoja na uhuni uliokuwa unaharibu demokrasia na uhuru wa nchi na vyama hivyo.

Alitoa mfano wa Kifungu cha 6 cha muswada huo ambacho kinatoa masharti ya chama kubadili Katiba yake kupitia Mkutano Mkuu na sio vinginevyo.

“Muswada huu, unakuja kuvifanya vyama vya siasa viendeshe shughuli zake kwa ubora zaidi na kulinda demokrasia. Kifungu cha Muswada cha 6, kifungu kidogo cha 1 hadi cha 5, kinaweka mambo ambayo yatavifanya vyama vya siasa vifanye kazi zake vizuri kwa kulinda demokrasia ya nchi na demokrasia ya vyama vyao,” alisema Mapunda.

Aliongeza kuwa muswada huo utawabana wale aliowaitwa ‘wahuni wachache’ waliokuwa wanaweza kubadili Katiba ya chama kwa maslahi yao binafsi.

“Hivi ni nani asiyejua, kulikuwa tu na utaratibu mtu akiona mwaka huu ni uchaguzi, mwaka huu nitaguswaguswa kama Mwenyekiti, basi hawahitaji Mkutano Mkuu, wanakaa wahuni wachache wanabadili Katiba. Sheria hii inakwambia mamlaka ya kubadili katiba ni ya Mkutano Mkuu,” aliongeza.

Alisisitiza kuwa endapo mazoea ya uholela uliofanywa tangu mwaka 1992 ulipoanza mfumo wa vyama vingi nchini utaruhusiwa kuendelea, basi uholela huo utakuwa ‘uholela halali’.

Akizungumzia hoja ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee aliyepinga chama cha siasa kuwasilisha rejista ya wanachama wake kwa madai kuwa idadi hiyo ni kubwa kuisimamia kutokana na wanachama kuingia na kutoka mara kwa mara, Mapunda alipinga hoja hiyo akitoa mfano wa CCM na Kanisa Katoliki.


“CCM ina wanachama milioni nane, na wote wako kwenye rejista. Kanisa Katoliki duniani, lina wafuasi wake dunia nzima na rejisti ya Wakatoliki wote iko Roma. Ni ajabu sana mwanasiasa anayetarajia kuwa kiongozi aseme kuwa na idani na majina ya wanachama wake ni jambo dogo. Hili sio jambo dogo hata kidogo,” amesema Mbunge huyo.

Mapunda ameungana na idadi kubwa ya wabunge hasa wa CCM ambao wamesema kuwa muswada huo umewasilishwa katika kipindi muafaka kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa vyama vingi na kupanua wigo wa demokrasia ndani na nje ya vyama vya siasa
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad