BUENOS AIRES, Argentina: GWIJI wa soka nchini Argentina, Diego Maradona (58), kwa sasa yeye na mpenzi wake wa zamani ni paka na panya, lakini ametoa kali baada ya kutamka kuwa kuna wakati nusura amkate kichwa mrembo huyo.
Maradona, hivi karibuni alitengana na Rocio Oliva, 28, na alikuwa amemzidi miaka 30 mrembo huyo.
Akizungumza na kituo kimoja cha redio nchini Argentina, Maradona alisema: “Mimi siyo mpigaji wa mke, lakini yule nilitaka kumkata kichwa.
“Alisaini makubaliano kwamba hatazungumza chochote. Hizo bata anazokula kwenye mapumziko yake, anafanya hivyo kwa pesa zangu. Sasa yupo nje kabisa ya maisha yangu.”
Wawili hao walimwagana hivi karibuni, baada ya miaka sita pamoja. Maradona amesema ataichukua nyumba aliyompa mrembo huyo jijini Buenos Aires.
“Nyumba niliyowapa familia yake ni yangu, nakwenda kuichukua. Samahani kama hawajui kumtunza mtoto wao. Mimi siyo Father Krismasi ambaye nazunguka mtaani kuwauliza watu wanahitaji nini. Nafanya kazi kama mtu yeyote yule duniani anavyofanya.”
Maradona aliongeza kuwa Oliva hayupo vizuri kichwani, na penzi lao limekufa.