Hisia na maoni mbalimbali yanaendelea kutolewa kuhusiana na matokeo hayo ya uchaguzi wa rais katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Ufarasa imeyapinga matokeo hayo ikisema kuwa ushindi uliotangazwa wa kiongozi wa upinzani Felix Tsisekedi hauendani na matokeo na kuwa mpinzani wake Martin Fayulu anaonekana kuwa ndiye aliyeshinda.
Katika matamshi yaliyotolewa saa chache baada ya matokeo ya awali kutangazwa, Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni Jean-Yves Le Drian alisema mpinzani wa Tsisekedi Fayulu, ambaye alitangazwa kupata nafasi ya pili, ndiye angetangazwa mshindi.
Le Drian amekiambia kituo cha televisheni cha Ufaransa CNews kuwa inaonekana matokeo yaliyotangazwa hayaendani na ukweli halisi, Amesema Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Congo – CENCO lenye nguvu kubwa, ambalo liliwatuma waangalizi karibu 40,000 katika maeneo mbalimbali kufuatilia uchaguzi huo, linajua nani hasa alishinda uchaguzi huo huku takwimu zao zikiashiria kuwa Fayulu ndiye aliyeshinda.