Mawakili wa Habinder Sethi na James Rugemarila Wataka Upelelezi Ukamilike


Upande wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili Habinder Sethi na James Rugemarila umeutaka upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi kwa kuwa kesi hiyo ipo kwa muda mrefu tangu Juni, 2017.

Rugemarila, ambaye ni Mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL na Sethi ambaye ni mwenyekiti mtendaji wa PAP, wanadaiwa kutenda makosa hayo katika jiji la Dar es Salaam na nchi za Afrika Kusini, Kenya na India.

Wakili wa utetezi, Michael Ngalo alidai mbele ya hakimu mfawidhi, Kelvin Mhina katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu wakati  kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

"Kesi hii ipo kwa muda mrefu hivyo tunauomba upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi ili washtakiwa waweze kupata haki yao kwa wakati," alidai Ngalo.

Hayo yameelezwa baada ya Wakili wa Takukuru, Leonard Swai kudai mahakamani hapo kuwa shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika hivyo kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Mhina baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 31, 2019 kesi hiyo itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Sethi na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi na kutoa nyaraka za kughushi.

Pia wanadaiwa kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad