Mawakili wa Serikali Wadai Mahakama haina mamlaka kusikiliza Kesi ya muswada wa sheria ya vyama vya siasa

Mawakili wa Serikali Wadai Mahakama haina mamlaka kusikiliza Kesi ya muswada wa sheria ya vyama vya siasa
Serikali imedai Mahakama Kuu ya Tanzania haina mamlaka ya kusikiliza shauri la kupinga muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Vyama vya Siasa.

Hoja hiyo imetolewa leo Ijumaa Januari 11, 2019 na kiongozi wa jopo la mawakili wa Serikali, Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo, wakati akiwasilisha hoja za pingamizi la Serikali dhidi ya usikilizwaji wa shauri hilo.

Wakili Mulwambo amedai katika dhana ya mgawanyo wa mamlaka katika mihimili mitatu ya dola kila mhimili uko huru kufanya shughuli zake bila kuingiliwa na mhimili mwingine.

Amedai Katiba inalipa Bunge mamlaka ya kutunga sheria kwa mujibu wa Ibara za 63 na 64 na kwamba pia katika hiyo Ibara ya 100 inalipa Bunge kinga ya kutokuingiliwa katika utekelezaji wa shughuli zake.

Amedai  Katiba inatoa uhuru wa maoni, uhuru wa mjadala wakati wa shughuli za Bunge na kinga ya kutoingiliwa katika utekelezaji wa majukumu yake.

Pia, Wakili Mulwambo amedai kifungu cha 8(3) Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi za Binadamu na Wajibu kinaizuia Mahakama kuingilia mjadala wa muswada.

Wakili Mulwambo amedai sheria na Katiba inatoa haki kila mtu kwenda mahakamani kupinga sheria anayoona inaathiri haki zake na si muswada kwani muswada si sheria hivyo hauwezi kumwathiri mtu kwa namna yoyote ile.

"Waombaji wameleta maombi haya chini ya Ibara ya 30 ya Katiba, lakini ibara hiyo inazungumzia sheria na si muswada. Hivyo Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza shauri Hilo.

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali, Abubakar Murisha amedai mmoja wa waombaji katika shauri hilo, Zitto Kabwe ni mbunge tena mzoefu anayezijua kanuni za Bunge.

Amedai kanuni ya 88 inampa haki mbunge kuomba muswada kusitishwa kwa muda mpaka atakapowasilisha mapendekezo yake, lakini hakuitumia fursa hiyo.

Amedai ingawa wadai wengine, Joran Bashange na Salim Bimani si wabunge lakini kanuni za Bunge zinawapa nafasi ya kutoa maoni yao.

Upande wa Serikali bado unaendelea kutoa hoja zake huku mawakili hao wakipeana zamu, kabla ya mawakili wa waombaji kijibu hoja hizo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad