Mawaziri Watano Watembelea Mradi Wa Kufua Umeme Stiegler's Gorge


Mawaziri Watano Watembelea Mradi Wa Kufua Umeme Stiegler's Gorge
Serikali imesema maandalizi ya miundombinu wezeshi kabla ya kumkabidhi Mkandarasi aliyepewa kazi katika Mradi wa kufua umeme wa Mto Rufiji tayari imekamilika kwa asilimia themanini.

Miundombinu hiyo ni pamoja na maji, umeme, barabara pamoja na  nyumba za kukaa wafanyakazi.

Kauli  hiyo imetolewa jana na Mawaziri wa Wizara tano  kutoka Nishati, Maliasili na Utalii, Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira,  Fedha na Mipango baada ya kutembelea na kujionea miundombinu hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa imeshakamilika.

Ziara hiyo katika Pori la Akiba la Selous kanda ya Matambwe mkoani Morogoro iliongozwa na Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani ikilenga kukagua hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa miundombinu wezeshi ili kumuwezesha Mkandarasi kuanza kusafirisha mizigo kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.

Alisema kukamilika kwa miundombinu hiyo kutamuwezesha Mkandarasi huyo kuanza maandalizi ya awali ikiwemo kuanza kusafirisha mizigo kuileta katika maeneo ya ujenzi wa bwawa.

Aliongeza kuwa kutokana na Mkataba uliopo Mkandarasi huyo ataanza kazi rasmi Juni 15 mwaka huu na ataukamilisha mradi huo ifikapo mwezi  April 2022.

Katika upande wake  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu alitoa tahadhari kwa wafanyakazi wanaokuja kufanya kazi katika mradi huo wasiende kupumzika vichakani kuna wanyama wakali kama vile Simba, Nyati pamoja na  tembo.

" Wale wenye tabia ya kujipumzisha vichakani baada ya kufanya kazi chonde chonde jiepusheni na haya mazoea la sivyo mtaliwa na Simba.

Aidha, Mhe.Kanyasu alitumia fursa hiyo kuiomba Wizara ya Utumishi kutoa kibali cha kuajiri Askari Wanyamapori zaidi ya 200 ambao watatoa ulinzi kwa Wafanyakazi wa mradi huo,

Ombi hilo linakuja kufuatia Askari wanyamapori 115 kutoka mapori mengine kuhamishiwa kwa muda  katika Pori hilo  katika kanda ya Matambwe kwa lengo la  kuongeza nguvu baada ya askari 115 waliokuwepo kuonekana hawatoshi.

Hata hivyo , Mhe.Kanyasu alisema  hatua za haraka zimeanza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja  kutengeneza  vyoo, malazi pamoja na maji kwa vile miundombinu iliyokuwepo katika Kanda hiyo ilikuwa na uwezo wa kuhudumia Askari Wanyamapori 85 tu lakini hadi hivi sasa kuna jumla ya askari 230.

Kukamilika kwa mradi huo wa kufua umeme, Bwawa hilo la Rufijin litakuwa la nne kwa ukubwa kwa Afrika na la kwanza kwa Afrika Mashariki, Duniani ni la 60 katika ya mabwawa sabini makubwa.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Bonge la synergy! Safi sana viongozi wetu, muendelee na moyo huo nawaombea kila leo afya ulinzi mshikamano hekima akili, hofu ya Mungu, utii na uzalendo na ulinzi wa family zenu naziombea pia

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad