Aidha, taasisi hiyo inakusudia kumfikisha mahakamani mfanyabiashara huyo kwa madai kuwa kitendo alichokifanya ni kosa kwa mujibu wa sheria na taratibu za uzalishaji wa mbegu.
Mfanyabiashara huyo anayefanya shughuli zake katika eneo la Uyole jijini Mbeya, alikamatwa jana wakati maofisa wa Tosci kutoka makao makuu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi walipofanya ukaguzi wa kushtukiza katika maduka mbalimbali ya mbegu jijini Mbeya.
Mkaguzi wa Tosc kutoka makao makuu, Emmanuel Mwakatobe, alisema mfanyabiashara huyo alikuwa anauza mbegu ambazo baadhi hazina nembo ya taasisi hiyo na zingine zikiwa hazina vielelezo vinavyoonyesha mahali alikozinunua mbegu hizo.
“Tunaendelea na ukaguzi huu katika nchi nzima na niwahakikishie Watanzania hatutaweza kuwavumilia wafanyabiashara wa aina hii, kwa sababu wanachangia kushuka kwa sekta ya kilimo na wanachafua kampuni zingine,” alisema Mwakatobe.
Vilevile Mwakatobe alisema sio mara ya kwanza kwa mfanyabiashara huyo kutuhumiwa kwa biashara hizo kwa madai kuwa awali wananchi walikuwa wanamlalamikia.