Mnyika Amvaa Spika Ndugai, Adai Bunge la Sasa ni Dhaifu


Zikiwa zimesalia siku nane kabla ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, kufika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kujieleza kuhusu kauli aliyoitoa kwamba Bunge ni dhaifu, Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika, naye amekoleza moto kwa  kusema Bunge la sasa ni dhaifu.

Mnyika alitoa kauli hiyo jana wakati wa mjadala ulioshirikisha vyama vya siasa kuhusu Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa ulioandaliwa na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), ulioongozwa na Rais wa chama hicho, Fatma Karume.

Alipoanza kuchangia, Mnyika aliwashukuru TLS kwa kuandaa mjadala huo na kuahidi kuwa maoni mbalimbali yaliyotolewa washiriki wa mkutano huo, Chadema itayachukua kwa ajili ya kusukuma mabadiliko ili hatimaye wahakikishe ile nia mbaya ya muswada huo haitimii.

“Nianze kwa kuwaeleza waziwazi na kuwaomba sana kwamba kwa muundo wa Bunge letu lilivyo sasa na kwa namna Bunge lilivyo dhaifu, tukifikiria kuwaachia wabunge na kuwaachia mchakato wa kibunge uendelee mpaka mwisho tukitarajia kwamba mambo mabovu yaliyoelezwa kwenye muswada yatabadilika, tutakuwa tunafikiria vibaya,” alisema Mnyika.

Mnyika aliwaomba washiriki wa mjadala huo wasiishie kutoa maoni yao hapo bali washirikishe taasisi za kidini na za kiraia ziende kwa wingi mbele ya Kamati Dodoma kufikisha ujumbe kwamba muswada huo usiende mbele ya Bunge badala yake uondolewe kabisa.

Januari 7, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alimtaka CAG afike mbele ya Kamati hiyo, Januari 21 kujieleza kutokana na kauli yake aliyoitoa Marekani wakati akihojiwa na redio moja nchini humo kuhusu Bunge linavyotekeleza mapendekezo ya ripoti zake.

Mbali na kumtaka Profesa Assad kufika mbele ya Kamati, Ndugai pia alimtaka Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, kuripoti mbele ya kamati hiyo, Januari 22, mwaka huu, kuthibitisha madai yake aliyoyatoa kupitia mitandao ya kijamiii kuwa Bunge ni dhaifu.


Aidha, Spika Ndugai aliongeza kuwa CAG na maofisa wake wanaingia kwenye Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).


Spika alifafanua kuwa ripoti hizo zikifika kwenye kamati hizo ambazo zinaongozwa na upinzani, muda wote maofisa wa CAG wanakuwapo kueleza upungufu waliobaini na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

Ndugai alisisitiza kuwa tangu serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani, imekuwa ikipambana dhidi ya matumizi mbaya ya fedha za umma na hatua zimekuwa zikichukuliwa.

Kadhalika, Ndugai alibainisha Bunge lilivyofanya kazi kubwa katika kipindi cha miaka mitatu tangu serikali ya Rais John Magufuli, ilipoingia madarakani mwaka 2015.



Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa (CCM), alisema mabadiliko makubwa kwenye usimamizi wa fedha za umma yamefanyika kwa ushauri wa Bunge na CAG, hivyo alishangazwa na hatua zipi ambazo CAG alitaka zichukuliwe.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad