MWEKEZAJI wa Simba Mohammed Dewji ‘Mo’ anatarajia kuteta na kocha mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems ili mikakati ya kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba imeingia katika hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kufuatia kuitoa timu ya Nkana FC ya Zambia kwa jumla ya mabao 4-3 nyumbani na ugenini.
Simba imepangwa kundi D, ambapo itaanza kucheza na JS Saoura ya Algeria, huku wakiwa pamoja na Al Ahly ya Misri na As Vita Club ya DR Congo, ambapo hatua hiyo ya makundi itaanza kuchezwa Januari 11 hadi Machi 17, 2019.
Aidha moja ya mikakati ya klabu ya Simba ni kufika hatua ya robo fainali.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Swedy Mkwabi amesema kuwa, uongozi wa klabu hiyo wakiongozwa na Mo unatarajia kukutana na Aussems mara baada ya kumalizika kwa sikukuu ili kupanga mikakati ya makundi.
“Mara baada ya makundi kupangwa bado hatujaamua cha kufanya, tunasubiria sikukuu ziishe ndipo tukutane na kocha Aussems ili kuweza kujadiliana naye juu ya michuano hiyo na tujue nini cha kufanya kwa kumpa mikakati yetu.
“Lengo la uongozi ni kuona tunafanikiwa kufikia malengo tuliyojiwekea baada ya yale ya kutinga hatua ya makundi sasa tunataka robo ama nusu fainali,” alisema Mkwabi.