Mahakama ya Hakimu Mkazi imewafutia mashtaka mfanyabiashara aliyetajwa na Rais John Magufuli kuwa alikuwa akiibia Serikali takriban Sh7 milioni kwa dakika, Mohamed Mustafa Yusufali na wenzake wanne.
Mfanyabiashara huyo na wenzake Alloyscious Gonzaga Mandago, Isaac Wilfred Kasanga, Taherali Sujjauddin Taherali na Mohamed Seif wanakabiliwa na mashtaka 198 ikiwamo ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo kwa mamlaka za Serikali, utakatishaji fedha na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh15 bilioni.
Washtakiwa hao wamefutiwa kesi hiyo, chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.
Wakili Mkuu wa Serikali, Hashim Ngole amedai mahakamani hapo kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa lakini Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hana nia ya kuendelea nalo dhidi ya washtakiwa hao.
Hakimu Augustina Mmbando amesema shauri hilo lilikuja chini ya kifungu namba 91(1) cha CPA, sura ya 20, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.
Hakimu Mmbando amesema kutokana na maombi hayo, mahakama hiyo imeifuta kesi hiyo.
Hata hivyo, washtakiwa hao baada ya kufutiwa kesi hiyo, wamekamatwa tena na kuwekwa mahabusu.