Katibu wa Baraza la Wazee wa Yanga, Mzee Ibrahim Akilimali amemgeukia aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Kelvin Yondani kwa kumtaka abadilike ili aweze kuendana na hali ya timu kwa sasa.
Hivi karibuni, kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera raia wa DR Congo alimvua unahodha beki huyo kutokana na madai ya utovu wa nidhamu ikiwemo kuchelewa kuripoti mazoezini baada ya mapumziko mafupi bila ya kuwepo kwa taarifa yoyote huku jukumu hilo akimpa mshambuliaji Ibrahim Ajibu.
Kwa mujibu wa gazeti la Championi, Mzee Akilimali alisema kuwa Yondani anapaswa kurekebisha tabia hiyo kutokana na ukubwa wake kwenye timu hiyo.
“Ni kweli Yondani kama ni kipenzi changu lakini katika masuala ya timu kocha ndiyo anajua na alichokifanya kwake anaona kipo sahihi siwezi kupinga maana kiongozi anapaswa kuwa mfano kwa wengine.
“Kikubwa nadhani anatakiwa ajirekebishe halafu anafahamu yeye ni nani ndani ya Yanga kwa sababu ukiangalia kwa wachezaji wakubwa kwa maana ya muda mrefu amebakia yeye na wachache ambao wanamuatia hivyo ni muhimu kuya fanyia kazi hayo,” alisema Mzee Akilimali.