Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, amemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, kuunda timu kutoka makao makuu itakayokwenda kushirikiana na wapelelezi wa Mkoa wa Njombe kuchunguza matukio ya mauaji dhidi ya watoto 10 mkoani humo.
Masauni alitoa agizo hilo jana, akiwa wilayani Njombe baada ya kukutana na waganga wa kienyeji kuzungumzia matukio ya mauaji dhidi ya watoto, yaliyohusishwa na imani za kishirikina.
Alisema timu ya IGP inatakiwa kuchunguza matukio yote ya mauaji mkoani humo na kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Agizo la pili IGP ahakikishe timu itakayotoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, inachunguza tukio la jana (juzi), lililosababisha polisi kutumia nguvu kwa kupiga mabomu ya machozi ili kutawanya wananchi, uchunguzi ujikite kubaini kiini na uwiano wa nguvu iliyotumika kuhusu uhalisia wa tukio," Masauni aliagiza.
Juzi, wakati naibu waziri huyo akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Njombe kwenye Viwanja vya Turbo, ghafla kulisikika milio ya mabomu ya machozi jirani na mkutano huo, kitendo ambacho kilisababisha taharuki na kusimama kwa mkutano huo.
Taarifa mbili zilizotolewa kwa Masauni kuhusu tukio hilo zilikinzana na kumfanya naibu waziri huyo kutaka uchunguzi ili kama amedanganywa, polisi wawajibike.
Katika agizo lake la tatu jana, Masauni alilitaka Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe kuongeza operesheni katika maeneo yote hususani kwenye mapori na misitu na kuhakikisha linakusanya taarifa za kiintelijensia ili kukomesha matukio hayo.
Kiongozi huyo wa serikali pia aliwataka Watanzania kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo, ili kukomesha vitendo vya uhalifu kwenye maeneo yao.
Naibu Waziri Amuagiza IGP Sirro Kuunda Tume ya Kuchunguza Mauaji ya Watoto Njombe
0
January 31, 2019
Tags