Naibu Waziri atangaza upungufu wa tani 260,000 za sukari Nchini

Naibu Waziri atangaza upungufu wa tani 260,000 za sukari Nchini
Serikali imesema taifa kwa sasa linakabiliwa na upungufu wa sukari, zaidi ya tani 260,000 ambazo zinapaswa kuwa sehemu ya mahitaji ya lazima kama nchi.

Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba amekiri kuwa upo upungufu wa sukari ya viwandani tani 155,000 na kwa sukari ya mezani, upungufu ni zaidi ya tani 105,000.

Mgumba alitoa taarifa kuhusu upungufu huo, wakati alipokwenda kujionea hali halisi ya uzalishaji wa sukari katika Kiwanda cha Sukari cha TPC Moshi.

“Tumeanza ziara ya siku sita mikoani na leo (jana), tumeanzia Kilimanjaro na kisha tutakwenda mikoa yote inayolima miwa ili kusikiliza, kupokea changamoto na kuzitatua kwa pamoja.

“Tutahakikisha tunamaliza upungufu huu wa sukari hapa nchini, wawekezaji tuelezeni sisi serikali changamoto zinazowakabili wakati wa uzalishaji ili tukae na kuona njia bora ya utatuzi wake, kuacha mazingira bora ya uzalishaji.”

Katika ukaguzi huo, Naibu Waziri Mgumba ameongozana na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Profesa Kenneth Bengesi.

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, mkurugenzi huyo ameeleza bayana kwamba bado mahitaji ya sukari hapa nchini ni makubwa na kuwataka wawekezaji waliowekeza katika viwanda vya sukari kuitazama fursa hiyo na kuifanyia kazi.

Kutokana na mahitaji hayo, Profesa Bengesi alisema: “Tumeweka mazingira rafiki ya wawekezaji kuwekeza katika sekta ya sukari, tunawakaribisha kwa sasa, serikali imedhamiria kuingia katika uchumi wa kati wa viwanda.”

Awali akitoa taarifa ya uzalishaji wa sukari kwa Naibu Waziri huyo, Ofisa Mtendaji Mkuu na Utawala wa TPC, Jafary Ally, alisema tangu walipowekeza katika kiwanda hicho wameweza kuongeza uzalishaji kutoka 36,000 hadi kufikia tani 110,000 kwa mwaka.

“Mawazo ya serikali ya kututaka kuzalisha sukari ya viwandani, tumeyapokea na tutakaa na bodi yetu kuona kama tunaweza kuwekeza katika sekta hiyo. Hata hivyo, tunaipongeza serikali kwa kuziba mianya yote ya uingizaji kiholela wa sukari kutoka nje, sasa wawekezaji wana uhakika wa soko,”alieleza Jafary.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad