Nairobi: Al-Shabaab wadaiwa kufungua vibanda 52 vya Simu-Pesa
0
January 25, 2019
Kesi dhidi ya watuhumiwa wengine sita wanaodaiwa kuhusika katika kufanikisha shambulizi la kigaidi lililofanywa na kundi la Al-Shabaab, jijini Nairobi imeendelea kuibua mshangao, baada ya kudaiwa kuwa maduka 52 ya M-Pesa yalifunguliwa kwa lengo la kusaidia uhamishaji wa fedha.
Watuhumiwa sita waliopandishwa kizimbani wanadaiwa kuhusika kwa namna mbalimbali kusaidia utekelezaji wa shambulizi hilo la Januari 15 mwaka huu katika eneo la 14 Riverside na kusababisha vifo vya watu 21.
Majina ya watuhumiwa hao ni Hassan Abdi Nur, Ismael Sadiq Abitham, Ali Khamisi Ali, Abdinoor Maalim Ismail, Abdullahi Mohamed Hassan na Sophia Njoki Mbogo.
Hassan Abdi Nur anadaiwa kumiliki maduka 52 ya huduma za M-Pesa, ambapo maduka 47 aliyafungua kati ya Oktoba na Desemba mwaka jana. Maduka hayo yameonekana kupokea fedha nyingi kutoka nchi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini na Somalia.
Muendesha mashtaka ameiambia Mahakama kuwa Ismael Sadiq Abitham, ambaye ni msimamizi wa akaunti za mitandao ya kijamii za kituo cha runinga cha Horizon, yeye alikuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na kiongozi wa shambulizi hilo, Salim Gichunge na mkewe Violet Kemunto.
Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama zilizotolewa kwa waandishi wa habari, Ali Khamisi Ali alikamatwa Jumanne wiki hii akihusishwa na kufanya mawasiliano ya mara kwa mara na raia wa Somalia wanaoaminika kuwa ni wafuasi wa Al-Shabaab, huku Ismael Sadiq Abitham akidaiwa kuwa na mawasiliano ya karibu na Gichunge na Kemunto.
Mwanafunzi wa masomo ya sheria, bdinoor Maalim Ismail ameshikiliwa kwa madai kuwa amekuwa na laini nyingi za simu zikiwa zimesajiliwa kwa jina lake huku akipokea jumla ya Sh100 milioni za Kenya (Sawa na Sh22.9 Milioni za Tanzania) kutoka kwa watu mbalimbali.
Sophia Njoki Mbogo ambaye ni meneja wa tawi la Diamond Trust Bank la Eastleigh yeye anashiliwa akishtakiwa kwa kutokutoa taarifa kuhusu kutolewa kwa fedha nyingi kwa mkupuo katika tawi lake, kinyume na sheria ya masuala ya fedha.
Muendesha mashtaka wa Serikali ameiomba mahakama hiyo kuruhusu washtakiwa kuendelea kushikiliwa kwa kipindi cha siku 30 wakati uchunguzi zaidi dhidi yao ukiendelea.
Juzi, Mahakama hiyo ilikubali ombi la upande wa mashtaka la kuendelea kushikiliwa kwa mtuhumiwa Zipporah Wambui Karanja, mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Kenya kwa madai ya kununua bima za magari mawili yaliyotumika katika shambulizi hilo.
Tags