Rapa Nay wa Mitego, amesema hawezi kuyumbishwa misimamo yake katika uimbaji na badala yake ataimba kwa kuangalia jamiii inataka nini ndiyo maana hata baada ya kupata matatizo kwenye wimbo wa wapo ameendelea kuimba na kusimamia anachokiamini.
Akizungumza na www.eatv.tv, kuhusu kutoa nyimbo mbili zinazokinzana (Alisema na Hakuna maisha magumu) kama ni kutokana na uoga au vitisho, Nay amesema katika maisha yake ya muziki hajawahi kuhofia na wala hafikirii kufanya hivyo kwa kuwa anaamini anachokifanya ni sahihi.
Msanii huyo amesisitiza kwamba, "Watu wanaongea kwenye wimbo wa 'Alisema' ulileta utata mwingi lakini Mwenyezi Mungu akatia mkono ukaendelea ku-'survive'. Hayakutokea yale waliyofikiria yanaweza kutokea".
Akizungumzia kuhusu Wimbo wa 'Hakuna maisha mugumu', Rapa huyo ameeleza kwamba aliangalia namna ambavyo vijana walikuwa wakilalamika na kukata tamaa na kuona kama maisha hayaendi kabisa hivyo mtu wa kumtoa katika mawazo hayo ni yeye msanii.
"Ndiyo maana nilisema hakuna maisha magumu. Unaweza ukala kwenye rambo mwenzio akala kwenye sahani lakini ukipambana hata wewe unaweza kula sahani. Hakuna kulala. Hivyo basi nilitoa maalumu kwa sababu ya vijana wenzangu siyo kwasababu nilisumbuliwa kwenye alisema" amesema.
Aidha Nay ameongeza kwamba, "Nilitoa wapo nikaenda mpaka jela, nikakamatwa na mitutu ya bunduki lakini niliendelea kufanya ninachokifanya. Ninaamini sifanyi kwa ubaya. nafanya kwa ajili ya kuweka vitu sawa, nikifanya makosa mimi ni binadamu ni mistake za kawaida tunatakiwa kurekebishana. So sina uoga huo naendelea na gemu yangu na hakuna kitakachobadilika".