Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, imekamata nguo zinazofanana za sare za kijeshi katika makambi ya wakimbizi.
Akizungumza na waandishi na kamati hiyo mjini hapa jana Alhamisi Januari 10, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Samson Hanga, alisema nguo hizo zilikamatwa Desemba 31 mwaka jana kati ya saa tano asubuhi hadi sita mchana kwenye makambi ya wakimbizi.
“Jumla ya nguo zinazofanana na sare za kijeshi 1,947 zilikamatwa katika kambi ya wakimbizi ya Mtendeli na Nduta zote za hapa hapa Kigoma.
“Katika Kambi ya Nduta zilikamatwa sare 1,325 na Mtendeli 622,” alisema.
Pamoja na mambo mengine, alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kuwabaini walioingiza sare hizo na lengo lao.