Mwanasheria wa supa staa wa klabu ya Juventus, Christiano Ronaldo ameeleza kuwa mamlaka ya polisi Jijini Las Vegas, nchini Marekani imeomba kibali cha kupata sampuli ya nyota huyo kwaajili ya uchunguzi wa kesi ya ubakaji inayomkabili.
Mwanasheria huyo aliyejulikana kwa jina la Peter Christiansen amesisitiza kuwa kibali cha DNA ya nyota huyo wa Juventus ni "ombi la kawaida " kati ya uchunguzi unaoendelea katika mashtaka hayo ya ubakaji.
Ikumbukwe kuwa karibia mwishoni mwa mwaka uliopita mwanadada raia wa Marekani, Kathryn Mayorga alimshtaki Ronaldo akidai kuwa alimdhalilisha kingono katika hoteli moja mjini Las Vegas mwaka 2009, kitendo ambacho Ronaldo amekipinga, akisema kuwa mwanadada huyo anajitafutia umaarufu.
Kwa mujibu wa mwandishi mmoja wa Kijerumani, Der Spiegel, taarifa ya kwanza ya madai hayo, Ronaldo alimlipa Mayorga kiasi cha Dola 375,000 mwaka 2010 kama sehemu ya makubaliano ya faragha na kumzuia kwenda kwenye umma na hata kushtaki.
Mayorga aliwasilisha mashtaka katika jaribio la kukomesha makubaliano hayo na kuitaka polisi wa Las Vegas kufungua upya uchunguzi.
"Kwa hiyo hii haishangazi kuwa hata DNA ingekuwepo, polisi wametuma ombi la kawaida kama sehemu ya uchunguzi wao", amesema Mwanasheria wa Ronaldo.