RAIS John Magufuli amewataka viongozi na watumishi wote wa serikali kuacha malumbano na badala yake kushirikiana katika kutekeleza miradi mbalimbali ili kuleta maendeleo kwa wananchi wote.
Magufuli amesema hayo leo Jumatano, Januari 9, 2019 baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua jana.
“Nilikuwa nafuatilia meseji za Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Katibu Mkuu wa TAMISEMI (Dkt. Zainabu Chaula) anayeshughulikia afya, nikaona wanavyorushiana maneno wee, mwigine ananyamaza lakini mwenzake anamshindilia maneno tu, nikasema hawa njia ya kuwakomesha ni kuwaweka wizara moja, akakae na dada yake. Wote wanatoka Tanga.
Akitoa mfano mwingine wa viongozi kutoelewana alisema:
“Nafahamu zipo halmashauri ambazo viongozi wanagombana mfano; Nyasa wanagombana sana DC na Mkurugenzi nimewaangalia tu! Nimewaachia kiporo chao. Kuna Gairo, DC na mbunge, mpaka mbunge ana-post ujumbe wa kumtukana DC tena mke wa mtu, hajui kama anaweza kupoteza ubunge… I hope siku moja ataomba msamaha kwenye Bunge.”
Mifano mingine aliyotoa ni ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma na Mkuu wa Wilaya ambao amewaonya na akasema “wamenyamaza naona yameisha.”
Pia Magufuli aliwachekesha wasikilizaji wake pale aliposema kwamba pamoja na mapungufu makubwa katika balozi za Tanzania, aliamua kumchukua aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya awe balozi kwa vile ameonyesha kusafiri sana kwenda nchi za nje.
“Tuna mapungufu makubwa katika balozi zetu, hivyo, ili kuimarisha hali hiyo nikaona nimchukue Katibu Mkuu wa Afya kwa sababu yeye ndiyo amesafiri sana kwenda nje. Nikaona bora akakae hukohuko nje. Wizara ya Afya ina mikutano mingi ya nje lakini jamaa hakutaka hata ku-delegate (kuwaachia wengine fursa ya kusafiri nje),” alisema Magufuli.
Aidha, aliwataka watendaji wasizichukulie wizara kama mali zao na wafanye maamuzi kwa maslahi ya nchi na kwa mujibu wa sheria.
Rais Magufuli: DC na Mkurugenzi Wanagombana Sana Nimewaangalia tu! Nimewaachia kiporo.
0
January 09, 2019
Tags