Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi aliyeapishwa jana kushika nafasi hiyo ameugua ghafla alipokuwa akitoa hotuba yake punde baada ya kula kiapo.
Hata hivyo, alirejea jukwaani badaye na kumalizia hatuba yake hiyo ya kwanza kama Amiri Jeshi Mkuu.
Imeelezwa kuwa hali hiyo ilitokana na uchovu alioupata kutokana na mchakamchaka wa kampeni pamoja na hali ya tukio la kuapishwa, kwa mujibu wa BBC.
Tshisekedi ambaye alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais wa Desemba 30 mwaka jana kwa tiketi ya chama cha upinzani cha Union for Democracy and Social Progress, ameapishwa kuwa Rais wa nchi hiyo akiandika historia ya kuwa wa kwanza kupokea madaraka kwa njia ya kidemokrasia tangu nchi hiyo ilipopata uhuru.
Hata hivyo, kutokana na kile ambacho wengi wanaamini ni vuguvugu la mvutano mkali wa uhalali wa kura zilizotangazwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Congo (CENI), tukio la kuapishwa kwake halikuhudhuriwa na viongozi wengi wa nchi za jirani.
Rais Uhuru Kenyatta, alikuwa Rais pekee aliyehudhuria tukio hilo la kihistoria akiambatana na Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga pamoja na Kalonzo Musyoka. Marais 17 walialikwa.
Mpinzani wa Tshisekedi, Martin Fayulu ameendelea kulalama licha ya kushindwa kesi ya kupinga matokeo ya urais mahakamani. Ameendelea kuwasihi wafuasi wake kuandamana kupinga Urais wa Tshisekedi kwa madai kuwa yeye ndiye aliyeshinda na kwamba Rais Joseph Kabila aliingia makubaliano na mpinzani wake huyo na kubadili matokeo.
Kwa mujibu wa CENI, Tshisekedi alipata kura milioni 7 ikiwa ni kura 400,000 zaidi ya alizozipata Fayulu aliyemfuatia.