Muungano wa maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC, umetoa wito wa kuundwa kwa serikali ya muungano nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia mzozo uliokumba matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika mwezi uliyopita.
Tangazo hilo limetolewa kupitia taarifa ya rais wa Zambia Edgar Lungu.
Hatua hii ya SADC inakuja siku moja baada ya mgombea wa upinzani katika uchaguzi mkuu uliyofanyika nchini Jamhuri ya kidemocrasia ya Congo amewasilisha kesi katika mahakama ya katiba kupinga matokeo ya uchaguzi huo.
Martin Fayulu amesisitiza kuwa alishinda uchaguzi huo lakini tume ya uchaguzi ikamtangaza mshindani wake Felix Tshisekedi kuwa mshindi.
Rais wa Zambia, Edgar Lungu, amesema kuwa wamezingatia "mvutano mkali uliyoibuka" kupinga matokeo ya awali.
Amesema viongozi wa kikanda wanaonelea njia mwafaka ya kusuluhisha mzozo huo ni kupitia muafaka wa kisiasa ambao utatoa nafasi ya kuundwa kwa serikali ya muungano wa kitaifa.
Bwana Lungu alitoa mfano wa mwafaka wa kisiasa uliopatikana nchini Zimbabwe na Kenya.
Waziri wa mambo ya nje wa Afrika Kusini,Lindiwe Sisulu, anapendekeza mchakato wa kisheria ufuatwe DRC kuhusiana na suala hilo huku akitoa wito kuwa watu wa nje wasiwalazimishe Wacongo jambo ambalo hawajaridhia.
SADC Yapendekeza Kuundwa Kwa Serikali ya Muungano DRC
0
January 14, 2019
Tags